Ofisi ya Msajili wa Hazina kufanya mambo mawili makubwa kila mwaka

NA GODFREY NNKO

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema, kila mwaka Ofisi ya Msajili wa Hazina itakuwa na matukio mawili makubwa ambayo yatakuwa yanahusisha viongozi wa Kitaifa.

Tukio la kwanza ni Siku ya Gawio kwa Serikali kutoka taasisi na mashirika ambayo yapo chini ya ofisi hiyo na tukio la pili ni mkutano wa wakuu wa taasisi na mashirika ya umma (CEOs Forum).
Mchechu ameyasema hayo leo Julai 15,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ambapo ametangaza kikao cha pili kati ya ofisi hiyo na wakuu wa taasisi na mashirika ya umma nchini kitafanyika mwezi ujao jijini Arusha.

Amesema, miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na taasisi hizo kuwekeza nje ya Tanzania huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mchechu amekumbushia kuwa, wakati Mheshimiwa Rais akifungua kikao chao cha kwanza mwaka jana jijini Arusha aliwaagiza kuanza kuangalia fursa za uwekezaji wa mashirika hayo ya Serikali nje ya nchi.

"Kama Ofisi ya Msajili wa Hazina tutakuwa na vikao viwili vikubwa kwa kila mwaka, ambavyo vinakwenda kugusa viongozi wa Kitaifa.

"Kikao au tukio la kwanza ambalo litakuwa linafanyika kila mwaka litakuwa ni kuhusu gawio kwa sababu hilo tukio la gawio kama lilivyofanyika tarehe 11 mwezi wa 6 mwaka huu, hii ni kwa taasisi zote kwenda kurejesha magawio yao kwa Mheshimiwa Rais au kutimiza wajibu wao wa kisheria. Hii itakuwa inafanyika kila mwaka.

"Tukio la pili ni kama hili la kikao tunachokwenda kufanya Arusha, nalo ni tukio la kila mwaka. Hivi ni vikao vyetu vikubwa sana vya matukio yetu mawili makubwa ambayo tutakuwa tunayapa umuhimu wake na yatakuwa na viongozi wa ngazi ya Kitaifa na moja lilishafanyika na Mheshimiwa Rais alikubali tukio la gawio la kila mwaka,na amekubali kuwa mgeni rasmi katika shughuli hii ya Arusha.

"Tunafikiri hizi mbili zinatutosheleza sisi kama Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwajibika kwa jamii yetu kwa namna ilivyo kubwa kwa Watanzania wote," amesisitiza Mchechu.

Amesema, kauli mbiu ya mkutano ujao itakuwa ni "Mikakati ya Mashirika na Taasisi za Umma kuwekeza Nje ya Tanzania".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news