OUT kuadhimisha miaka 30 kwa namna yake nchini

NA GODFREY NNKO

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimezindua maadhimisho ya miaka 30 tangu kianze kudahili wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka 1994.
Uzinduzi huo umefanywa leo Julai 18,2024 na Makamu Mkuu wa chuo hicho,Prof. Elifas Tozo Bisanda katika makao makuu ya chuo yaliyopo Kinondoni Biafra jijini Dar es Salaam.

Prof.Bisanda amesema, maadhimisho hayo kilele chake kitakuwa Novemba, mwaka huu wakati wa Mahafali ya 43 ambayo yanatarajiwa kufanyika mkoani Kigoma.

"Vitivo, vituo vya mikoa, kurugenzi, idara na wadau mbalimbali watashiriki kikamilifu katika kuandaa maonesho, mihadhara ya wazi na shughuli mbalimbali za maadhimisho."

Prof.Bisanda amesema, baadhi ya shughuli zitakazofanyika kama sehemu ya maadhimisho hayo ni kuandaa mihadhara ya umma na makongamamo ya wanazuoni ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa na kujadiliwa.

Vile vile, amesema yatafanyika maonesho ya kitaaluma ambayo yataandaliwa na kuratibiwa na vitivo zikiwemo kurugenzi na vituo vya mikoa.

"Pia kutakuwa na Wiki ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ambapo wanasheria watatoa msaada wa kisheria, ushauri na elimu kwa wananchi."

Prof.Bisanda ameongeza kuwa, kupitia maadhimisho hayo litafanyika Kongamano la Kimataifa la Elimu ambalo litawakutanisha watafiti na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.

"Kongamano hilo la Kimataifa ni la pili kuandaliwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kupitia Kitivo cha Elimu ambapo mwaka huu linaandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya chuo huku mada yake kuu ikiwa ni Kuendeleza Elimu ya Msingi kwa Maendeleo Endelevu na inaendana na kauli mbiu ya maadhimisho."

Hata hivyo, maadhimisho hayo ya miaka 30 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yanaongozwa na kauli mbiu ya 'Miaka 30 ya Kufungua Fursa Endelevu za Elimu kwa Njia ya Masafa na Huria'.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. We are asking for the 0FP results that the application window is now open

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news