DAR-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Havard kutoka Marekani pamoja na wadau wengine wanatarajia kutekeleza mradi wa uwekaji darubini Mlima Kilimanjaro.
Mradi huu utaongeza fursa za kiutalii na kuleta manufaa ya kiuchumi katika nchi yetu ikiwemo kuongeza idadi ya watalii, kuvutia wanafunzi na watafiti kutoka nje ya nchi kuja kujifunza na kutalii anga za juu kwa kutumia darubini hiyo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na wadau mbalimbali wa darubini ya Mlima Kilimanjaro, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Prof. Elifas Tozo Bisanda amesema darubini au kiona mbali kitawekwa katika eneo la tambarare lililopo kati ya Kibo na Mawenzi katika Mlima Kilimanjaro ili kuongeza fursa za utalii wa Anga.
"Watalii wataweza kutalii zaidi, badala tu ya kuuona mlima wataweza kuona nyota na sayari mbalimbali hivyo kuongeza fursa za kitalii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini hasa katika sekta ya utalii", alisema Prof. Bisanda na kuongeza;
“Mradi huu pia unalenga kuleta fursa ya kuanzisha Kituo cha Tafiti ya Sayansi ya Anga katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, hivyo tumekutana hapa na wadau mbalimbali kupata maoni yao, kujadili na kuwaelewesha zaidi kuhusu mradi huu kwani wakishaelewa unawanufaisha wao pia basi watauunga mkono”.
Naye mwanzilishi wa “Event Horizon Telescope” kutoka Chuo Kikuu cha Havard Marekani Bw. Sheperd Doleman amesema mradi huu utaleta ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Marekani kwani utafungua fursa mbali mbali za kielimu na kiteknolojia baina ya nchi hizi mbili.
“Tumekuja Tanzania kutumia fursa hii kuchunguza na kujua ni darubini ipi itafaa katika Mlima Kilimanjaro kusaidia watu kuona hata ndani ya mawingu pamoja kuongea na wadau kuhusu jiografia ya mkoa, tamaduni na kila kitu kinachohusiana na Mlima huo,” amesema Bw. Sheperd.
Naye Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi TANAPA, Bw. Bakari Mnaya amesema mradi huu unatarajiwa kufanyika katika Mlima Kilimanjaro ambao ni sehemu ya hifadhi ya taifa ya Kilimanjaro. Hii itaongeza thamani ya mlima katika eneo zima la vivutio vya utaliii na elimu pia hivyo ni kitu kizuri kitakacholeta mafanikio katika nchi yetu.
Akiongeza Mtaalamu wa Astronomia na Mwenyekiti wa Chama cha Astronomia nchini Dkt. Noorali Jiwaji amesema Darubini hii ikikubaliwa italeta uwekezaji mkubwa wa kiuchumi kwa kuiinua sayansi na elimu na vilevile jamii kuamka katika nyanja za sayansi na teknolojia.
Akihitimisha, Prof. Alex Makulilo ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Huduma za Ushauri wa Kitaalamu amesema mwaka huu Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinaadhimisha Miaka 30 ya chuo na hivyo sehemu hii ya utafiti huu wa Anga ni sehemu ya maadhimisho haya na hivyo tukio hili linakuwa ni tukio muhimu katika chuo chetu.
Mkutano huu umefanyika Marangu mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na wataalamu kutoka Chuo kikuu Huria cha Tanzania pamoja na wadau wengine mbalimbali wa maswala ya anga wakijadili namna bora ya utekelezaji wa mradi huo.