OUT yazindua Kamati ya Ushauri wa Kitasnia

DAR-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimezindua rasmi Kamati ya Ushauri wa Kitasnia (Industrial Advisory Committee) ambapo kamati hiyo itakuwa na jukumu la kukishauri chuo katika masuala ya kitaalam na pia kuunganisha chuo na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Juni 28, 2024 katika viwanja vya Makao Makuu ya Chuo, Kinondoni Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Peter Msofe kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Caroline Nombo, amesema, OUT imepiga hatua kubwa kufanikisha uzinduzi wa kamati hii muhimu ambayo kazi yake kubwa ni kukishauri chuo katika maeneo mbalimbali ili kutoa huduma nzuri za viwango vya juu kwa Watanzania.
“Kamati hii itatoa ushauri katika maeneo ya utafiti, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ushauri wa kitaalamu. Wizara ina matumaini kuwa OUT itatumia kikamilifu kamati hii kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya Chuo na taifa,” amesema Prof. Msofe.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema Kamati hii ni muhimu kwa chuo kwa kuwa itakuwa kiunganishi cha Chuo na viwanda, sekta za umma na binafsi, jamii na wadau mbalimbali wa elimu nchini.“Katika ulimwengu tuliopo elimu ujuzi ndiyo suluhisho la ukosefu wa ajira nchini, ushirikiano baina ya taasisi za elimu ya juu na sekta binafsi ni chachu ya kufanikisha hilo. Tunahitaji kuwa na wahitimu wenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine na ili hili lifanikiwe lazima tuwe na ushirikiano wa karibu na viwanda ili wanafunzi wetu waweze kupata nafasi za mafunzo kwa vitendo,” amesema Prof. Bisanda.
Akizungumza katika uzinduzi huo, mratibu wa Kamati za ushauri wa Kitasnia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hadija Kweka, amesisitiza kwamba ni hitaji la mradi wa HEET kila taasisi nufaika wa mradi kuwa na kamati hii ili malengo ya mradi yatimie pale utakapokamilika.

Kwa upande wake mratibu wa ushirikiano baina ya OUT na wadau Dkt. Angaza Gimbi amesema kilichobaki sasa ni kamati kutimiza wajibu wao kikamilifu. Katika kuhakikisha hilo linafanyika, ameahidi kushirikiana kwa karibu na Kamati pamoja na Menejimenti ya OUT ili hatimaye malengo makubwa ya uimarishaji mitaala, kuongeza ubunifu na ugunduzi Chuoni yaweze kufikiwa.
Uzinduzi kwa Kamati ya Ushauri wa Kitasnia umefanyika wakati muafaka ambapo hivi sasa OUT ipo katika mapitio ya Mitaala yake na hivyo ushauri kutoka katika kamati hii ni muhimu sana na utaongeza ufanisi na tija katika kutoa Mitaala bora na wahitimu watakaokuwa bobezi, bunifu na wenye kujitegemea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news