PPAA yajivunia Moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa kielektroniki

DAR-Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, Sheria hiyo imesaidia PPAA kuanzisha Moduli ya kuwasilisha Malalamiko na Rufaa kieletroniki, ambapo Moduli hiyo inapatikana katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kieletroniki (NeST).
Mafanikio hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando alipotembelea banda la PPAA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.Bw. Sando amesema mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, yamepelekea PPAA kuanzisha Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa zitokanazo na michakato ya zabuni kieletroniki.

“PPAA kwa kushirikiana na PPRA tumeanzisha Moduli hiyo ambayo inapatikana katika mfumo wa NeST,” alisema Bw. Sando.
“Kuanzishwa kwa moduli hiyo kuna faida kadhaa ikiwa ni pamoja na kuokoa muda, gharama na kuongezeka kwa wazabuni,” aliongeza Bw. Sando

Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando amesema Mamlaka hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Kanuni za Ununuzi wa Umma za Uwasilishaji wa Rufaa za Zabuni za Umma za Mwaka 2024.
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi ya Umma Na. 3 ya mwaka 2001 ambapo baada ya Sheria hii kufutwa, Mamlaka ya Rufani iliendelezwa chini ya Sheria ya Ununuzi ya Umma Na. 21 ya mwaka 2004 na kuhuishwa tena kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 baada ya ile Sheria Na. 21 ya mwaka 2004 nayo kufutwa. Mwaka 2023 Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 nayo ilifutwa na Mamlaka ya Rufani ilihuishwa tena kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news