Prof.Janabi aeleza kwa simanzi yanayowakuta watumiaji wa dawa za kulevya, mfumo wa umeme wa moyo unakata ghafla

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi amesema,tangu hospitali hiyo ilipoanzisha Kliniki ya Methadhone mwaka 2011 hadi kufikia Juni,2024 jumla ya waraibu 3,840 wameandikishwa kupata huduma ya Methadone.
Kati yao wanaume ni 3,692 na wanawake 148 ambapo waraibu 900 wanaohudumiwa kila siku kunywa dawa ya Methadone kati yao wanawake ni 30.

Dkt.Janabi ameyasema hayo Julai 17,2024 wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) jijini Dar es Salaam.

Amesema,changamoto iliyopo kwa sasa ni pale watumiaji wa dawa za kulevya wanapofika hospitali huku wakishindwa pa kuanzia kutokana na mchanganyiko wa dawa za kulevya.

"Tukichukulia sisi kiafya, kila dawa inayotengenezwa au tunazotumia sisi kwenye mahospitali yetu inayotumika hapa nchini kwanza lazima iwe imepita na kupata kibali cha TMDA,kwamba ni dawa iliyopimwa, nini faida yake, ile mimi ukipata mfano athari ya Asprin ninajua nikupe dawa gani kuweza kudhibiti ile Asprin.

"Sasa bahati mbaya sana tatizo tunaloliona sasa hivi kwa wale ambao wanakuja kwetu kupata tiba ya dawa za kulevya hospitalini wanatushangaza na hatujui tunawatibu kwa namna gani, maana hatuelewi mchanganyiko wa dawa waliotumia.

"Kwa sababu ni mchanganyiko ambao hata sisi hatuuelewi na athari yake sasa tunachokiona siku hizi kwanza hizi dawa zinaingiliana na mfumo wa umeme wa moyo.

"Ndiyo maana tunapata vijana wengi wanaotumia hizi dawa unasikia katumia overdose amefariki ghafla kwa sababu ule mfumo wa umeme wote unakuwa umechanganyikiwa.

"Pia athari kubwa inaweza kukupata kwenye figo. Pale Muhimbili tunasafisha figo wagonjwa 150 kwa siku kuna sessions tatu tu. Kuna session inaanza saa tisa usiku inakwisha saa nne.

"Kuna session inaanza saa sita inakwisha kwenye saa tisa, halafu kuna session ya mwisho inayokwisha saa mbili usiku."

Amesema sababu kuu tatu za wagonjwa wanaowaona Muhimbili ni, "Kwanza ni figo zilizokufa kwa sababu ya shinikizo la damu kwa sababu ya kisukari na magonjwa mengine.

"Lakini inayofuatia ni matumizi mabaya ya dawa za kulevya. Sasa mbali kwamba ni gharama ile quality ya maisha yako inakuwa imeharibika kabisa.
"Wanapataje saratani hawa watumiaji wa dawa za kulevya? Changamoto yao kubwa aidha kwa kushirikiana sindano au vitu vingine wanapata ugonjwa wa homa ya ini.

"Ukilinganisha kwa mfano ugonjwa wa homa ya ini na ugonjwa wa UKIMWI. Ugonjwa wa homa ya ini ni mara 10 zaidi kwa hatari ukilinganisha na UKIMWI sasa hawa vijana wakishapata ugonjwa wa ini.

"Ukipata ugonjwa wa ini baadhi yao wataishia kupata saratani ya ini mbali ya athari tunazoziona kwenye afya ya akili kwa sababu pale unapokuwa na dawa za kulevya kwenye mwili, afya yako ya akili lazima iharibike kwa sababu utapata brain insult na hata ukiwapiga hawa wagonjwa MRI unaona yale mabadiliko yanayotokea kwenye kichwa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news