NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof.Najat Kassim Mohammed ameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, uwekezaji ambao umeifanya taasisi hiyo kutoa tiba kwa kutumia mionzi nchini.Pongezi hizo amezitoa leo Julai 9,2024 jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika taasisi hiyo yenye ushirikiano wa karibu na TAEC katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku.
Amesema, huo ni mwendelezo wa ziara zake kwa taasisi ambazo TAEC wanashirikiana nazo na kuendesha miradi.
"Kwa hiyo tumepita leo hapa kuja kujifunza, kuona nini kinaendelea na kwa hakika tumeona Ocean Road wamepiga hatua kubwa sana katika mambo ya tiba ya kutumia mionzi na radiolojia.
"Leo nimejifunza hapa Ocean Road panaweza pakawa mfano wa taasisi ambayo inatumia vema hii Sayansi ya Mionzi na imepiga hatua kutoka katika matumizi ya kikale kwenda katika matumizi ya kisasa kabisa.
"Tunaishukuru Serikali, kwa sababu vifaa hivi vingi pia vimenunuliwa na Serikali yetu yenyewe, kwa hiyo tunashukuru kwa jitihada hizo.
"Lakini, pia tunaiomba Serikali kwamba hapa baada ya vifaa vyote hivi kunahitajika kuwa na wataalamu ambao wataweza kutumia hivi vifaa ipasavyo."Kwa hiyo,ni vema wakaongezewa kidogo ajira ili wapatikane vijana ambao wanaweza wakaziendesha hizi mashine bila kutegemea watu wa nje."
Pia, ameahidi kuendeleza ushirikiano ambao ulikuwepo awali na kuhuisha MoU za kisasa ili kupata maatokeo bora zaidi.
"Kwa sababu, TAEC inahusika na kuangalia matumizi haya ya mionzi, kudhibiti na kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi."
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ni taasisi iliyoundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003) inayoipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia nyuklia hapa nchini.
Lengo ni ili kulinda wafanyakazi, wananchi, wagonjwa na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.
Ocean Road
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Julius Mwaiselage amesema, lengo la ugeni huo ni kuweza kuona huduma ambazo kama taasisi wanazitoa katika maeneo mbalimbali hasa kwenye eneo la radiolojia na tiba mionzi.
"Kama mnavyojua, Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania inasimamia sana katika maeneo ya nguvu za atomu.Na sisi kama taasisi tunatoa huduma mbalimbali kwenye upande huo wa radiolojia, tiba ya nyuklia pamoja na tiba ya mionzi.
"Kwa hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof.Najat Kassim Mohammed amefika, tumemwelezea kuhusu huduma ambazo tunazitoa katika taasisi ya Ocean Road kwa wagonjwa."
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC amepitishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika eneo la mashine za X-rays, CT Scan na MRI.
"Lakini, pia katika mashine za uchunguzi za nyuklia ikiwemo mashine ya Maga Camera pamoja na mashine ya PET CT Scan ambayo ni mashine mpya kabisa ya kisasa pamoja na kiwanda chake."
Lakini, pia ameweza kujionea katika eneo la tiba za mionzi ambazo tunazitoa kupitia mashine za kisasa za Linear Accelerator au LINAC, lakini kubwa ni kwamba kuna ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pamoja na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC)."
Dkt.Mwaiselage amesema,katika maeneo mengi, "TAEC wanatusimamia sisi katika utoaji wa huduma, lakini pia amekuja kuona uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali hasa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwani ameweza kuwekeza katika vifaa mbalimbali vya uchunguzi wa saratani ambapo hapo awali, vilikuwa havipo na wagonjwa walikuwa wanaenda Muhimbili (Hospitali ya Taifa Muhimbili) kwa ajili ya kwenda kupata vipimo hivyo, lakini sasa hivi tunaweza kutoa huduma ya CT Scan hapa hapa, huduma za MRI hapa hapa.
"Lakini, kubwa pia uwekezaji katika upande wa tiba za saratani, mashine za Linear Accelerator zimesaidia kuongeza wagonjwa kutoka nje ya nchi."Kwa mwaka tunaona kwamba wagonjwa 514 ambapo ni kwa takwimu za mwaka jana ambao walitoka nchi za jirani ikiwemo Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Msumbiji na Comoro.
"Ambao wanakuja kufuata huduma hapa Tanzania, kwa sababu huduma ambazo tunazitoa ni huduma za kisasa na za kibingwa kabisa ambazo, baadhi ya nchi hawana huduma hizo."
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt.Julius Mwaiselage amesema, taasisi hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa TAEC ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
"Kwa hiyo, tumeshukuru kama wenzetu wanatusaidia kwenye maeneo ya mafunzo, lakini pia wao ndiyo wanaowasiliana na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (International Atomic Energy Agency (IAEA),kwa hiyo tumewapatia pia baadhi ya mahitaji yetu watusaidie kutufikishia kule.
"Na pia, kuendelea kupata mashine nzuri na za kisasa zaidi za Kitanzania ikiwemo katika upande wa tiba za mionzi kuna baadhi ya maeneo tumehitaji kupatiwa, lakini pia maeneo ya mafunzo ili kuendelea kujenga uwezo zaidi wa watumishi wetu katika Taasisi ya Ocean Road."Kwenye maboresho ya huduma ambazo zinapatikana katika taasisi yetu ya Ocean Road kama nilivyosema tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita, kwenye upande wa upatikanaji wa dawa. Dawa zote za saratani zinapatikana, asilimia 100 ya dawa zinapatikana.
Kwa hiyo, mgonjwa haitaji kwenda kununua dawa yoyote nje ya taasisi. Lakini, la pili kwenye upande wa tiba za mionzi tuna mashine za kisasa kabisa za kutibu saratani kwani tuna mashine za 3d. Hizi ni mashine ambazo tiba yake inapatikana katika hospitali yoyote kubwa duniani.
Kwa sababu yenyewe inalenga jinsi ulivyo. Uvimbe ulivyo kwa hiyo inaendana na uvimbe ulivyo, ni mashine za kisasa kabisa na mgonjwa yeyote anaweza kupata huduma yake katika taasisi yetu.
"Lakini, pia katika upande wa uchunguzi, mashine za CT Scan za uchunguzi zinapatikana, MRI zinapatikana lakini kubwa kabisa ni mashine ya PET CT Scan hii ni mashine ambayo inaweza kugundua saratani katika hatua ya awali kabisa kabla hata uvimbe haujajitokeza, zinapatikana hapa.
"Kwa hiyo, pia tungependa kuwaasa wananchi wawe na utaratibu wa kuzichunguza afya zao mapema, kwa sababu saratani ikigundulika mapema inaweza ikatibika na ikapona kabisa na tunaweza kuona uwekezaji ambao umefanyika kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania, waje kufaidika na huduma za tiba za saratani hapa nchini na wanakuwa hawana haja ya kwenda nje ya Tanzania."
Tags
Afya
Habari
Taasisi ya Saratani Ocean Road
TAEC Tanzania
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC)