WASHINGTON-Rais wa Marekani, Joe Biden mwenye umri wa miaka 81 amesitisha kampeni zake baada ya kugundulika ana UVIKO-19.
Picha na Aljazeera.
Julai 17,2024 Rais huyo alionekana akiwatembelea wafuasi wa chama chake huko Las Vegas na kuzungumza katika hafla iliyokuwa imeandaliwa mjini humo.
Hata hivyo, baadaye alifuta hotuba ya kampeni usiku kutokana na changamoto hiyo ya kiafya.
Daktari wa Rais huyo, Kevin O’Connor alisema, Biden alikuwa na dalili za matatizo ya kupumua, ikiwa ni pamoja na mafua na kikohozi na alipewa dozi yake ya kwanza ya Paxlovid.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, Kiongozi wa walio wengi katika Seneti, Chuck Schumer na Kiongozi wa walio wengi katika Bunge, Hakeem Jefferies walikutana na Biden kwa faragha.
Wanademokrasia hao wawili wakuu katika Bunge la Marekani kwa nyakati tofauti walimweleza kuwa, kuna uwezekano mgombea wao akaathiri ushindani katika Bunge na Seneti.
Ikulu ya Marekani White House imesema,Rais Joe Biden amegundulika kuwa na virusi vya UVIKO-19 na kuonesha dalili za athari za wastani za virusi hivyo.
Msemaji wake, Karine Jean-Pierre amesema, Biden aliyekuwa tayari amepata chanjo hiyo na kadhalika ile ya kuongezewa nguvu alijihisi hali isiyo ya kawaida.
Jean-Pierre amesema, rais alipanga kujitenga nyumbani kwake huko Delaware huku akitekeleza majukumu yake yote kikamilifu wakati huo.