ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo kuhakikisha kuwa biashara katika Soko la Kimataifa la Kariakoo zinafanyika saa 24 pindi ujenzi wa soko hilo utakapokamilika.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa agizo hilo leo Julai 5,2024 wakati wa hafla ya uapisho wa
viongozi wateule iliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu jijini Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt. Samia pia amemuagiza Waziri Dkt. Jafo afanye kazi kwa ukaribu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Mipango na Uwekezaji pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kusimamia sekta ya biashara katika soko hilo.

Katika kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa, Rais Dkt. Samia amemuelekeza Waziri Dkt. Jafo kufuatilia utoaji wa leseni kwa wazawa na wageni ikiwa ni pamoja na kusajili wafanyabiashara na kuwa na kanzi data yao.


Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amemuelekeza Kamishna Mwenda kuhakikisha wafanyabiashara wote nchini wanatumia Mashine za Kielektroniki (EFD) na kuwahamasisha wananchi kudai risiti kwa manunuzi wanayofanya.
Katika hafla hiyo, viongozi hao walioapa ni Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Mb),Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji ,Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Ismail Samamba na CPA Yusuph Juma Mwenda ambaye ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Tags
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Soko la Kimataifa la Kariakoo
TRA Tanzania
Wizara ya Viwanda na Biashara