NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi mkoani Katavi kwa namna ambavyo wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kupitia sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa pongezi hizo leo Julai 13,2024 wakati akisalimiana na wananchi wa Inyonga wilayani Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne mkoani humo.
"Ninawapongeza Wanamlele na Wanakatavi kwa ujumla kwa kwa kazi kubwa...kubwa mnayofanya, lakini ninawapongeze kwa maendeleo, kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi toka jana tumeingia ndani ya mkoa huu tumesikia taarifa ya mkuu wa mkoa kwenye utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwenye sekta zote, Afya,Elimu,Maji, Umeme,Kilimo. Sekta zote mambo Katavi ni mazuri mno.
"Lakini,tumekuja hapa tumemsikia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hili,jinsi alivyosema maendeleo yalivyopatikana katika jimbo lake na ninaamini majimbo mengine ni hivyo hivyo.
"Sasa ndugu zangu maendeleo ni hatua, tumefika hatua hiyo,lakini Serikali yenu itaendelea kuleta maendeleo zaidi na zaidi.
"Ndugu zangu tupo Katavi kwa ziara mbili,moja ziara ya kiserikali,lakini ya pili kufunga Wiki ya Jumuiya ya Wazazi ambayo ufunguzi wake ulifanyika hapa Mlele."
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani humo ambapo atakagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.