KATAVI-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi (132kV) pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme vinakamilika kwa wakati ili Mkoa wa Katavi uingizwe kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.



Amesisitiza kuwa, umeme ni tegemeo kubwa kwa watu binafsi pamoja na uchumi wa viwanda na hiyo yote ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza uwepo wa umeme wa kutosha nchini.
Alikiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Mhe. Rais, Mkurugenzi Mtandaji wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema, mradi huo pindi utakapokamilika utaokoa kiasi cha takribani Bilioni 2.2 kwa mwezi kwa ajili ya mafuta yanayotumika kuendesha Mitambo ya Umeme inayotumiwa mkoani Katavi pindi tu itakapoingizwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.