ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Ismail Samamba kwenda kushirikiana vema na Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Anthony Mavunde ili sekta hiyo iendelee kuleta matokeo chanya kwa ustawi bora wa Taifa.
"Nimefurahi kukujua leo maana nilikuwa nakusikia tu hongera kwa kuwa Katibu Mkuu. Waziri yuko pale najua mtakwenda kufanya vizuri.
"Wewe nimekutoa Tume ya Madini maana niliambiwa umefanya kazi nzuri sana, kwa hiyo nafasi yako ya Katibu Mkuu unaijua Tume vizuri najua utaisimamia vizuri;
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Julai 5,2024 katika Ikulu ndogo iliyopo Tunguu jijini Zanzibar wakati akiwaapisha wiongozi wateule.
Viongozi hao aliowaapisha ni Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo (Mb) ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Wengine ni Mhandisi Yahya Ismail Samamba ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Bw. Yusuph Juma Mwenda kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
"STAMICO tumefanya uwekezaji mkubwa sana na wamefanya vizuri, walipata zawadi kutokana na kufanya mageuzi makubwa na hata kwenye utoaji wa gawio kwa Serikali kwa hiyo nenda ukawasimamie vizuri shirika lisonge mbele.
"Kinachoniumiza kichwa ni kwenye leseni, mmetoa leseni nyingi watu wameshikilia lakini hakuna uwekezaji hakuna chochote kinachoendelea, nenda kalisimamie hilo.
"Waziri na mwenzie walishaanza kuangalia nani amefanya nini, nani ana nia na ana uhalali gani, nenda kalisimamie hilo.
"Sasa hivi nimetoka kuzungumza na Rais wa Benki ya Uwekezaji wa Europe (Ulaya) ananiuliza vipi huko madini kuna nini?.
"Nimemwambia tumefanya utafiti wa kina kwa asilimia 16 tu kwa nchi nzima kama mnaweza mtusaidie kwenye hilo ili tujue tuna nini kwa kiasi gani. GST iongezewe nguvu ifanye tafiti za madini maeneo yote.
"Wachimbaji wadogo huko nyuma tulikuwa tunawaona kama kero lakini wameibeba Sekta. Juzi niliona taarifa ya kutoroshwa kwa madini ya dhahabu kutoka Afrika ya zaidi ya dola bilioni 35.
"Nenda kasimamie mapato ya dhahabu yarudi nchini, hatuna sababu ya kulia kwa kukosa dola.Hitimisho, ninawapongeza na ninawapa pole kwa kuamininiwa, mkafanye kazi kama sheria zinavyotaka uongozi ni dhamana."