DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayowataka kuwathamini na kuwaheshimu wananchi.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Ikulu, wakati akiwaapisha Viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Balozi.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amemuagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa kuendelea kusimamia kikamilifu uhuru wa habari kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.

Vile vile, Rais Dkt. Samia amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia Wizara za kisekta kama vile kilimo, mifugo, uvuvi na madini.

Kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Dkt. Samia amemtaka Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuboresha utendaji na kulinda heshima ya nchi kimataifa.