KIGALI-Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame na Mgombea Urais kupitia RPF amepata ushindi wa kimbunga.
Ni katika uchaguzi ambao utaongeza muda wa utawala wake kwa miaka mingine mitano, kulingana na sehemu ya matokeo yaliyotolewa Julai 15,2024.
Aidha,kama kiongozi mkuu tangu mwisho wa mauaji ya kimbari ya 1994 na rais tangu 2000, Mheshimiwa Paul Kagame amepata asilimia 99.15 ya kura ikiwa ni zaidi ya matokeo ya mwaka 2017 ambayo alipata asilimia 98.79.
Hayo ni kwa majibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda ambayo ilitangaza matokeo hayo baada ya asilimia 79 ya kura kuhesabiwa.
Akiwa huko Rusororo, Mheshimiwa Paul Kagame alinukuliwa akisema, "Mchakato huu wa uchaguzi, kampeni tulizofanya kwanza, upigaji kura, na matokeo ambayo yametoka tu na kutolewa, yanamaanisha kitu muhimu katika maisha ya mtu.
"Hii inaashiria uaminifu, ambao ninawashukuru. Kuaminiana si jambo rahisi, hakuna kitu unaweza kumpa mtu ili kupata imani yake ya haraka. Uaminifu hujengwa kwa muda.
"Kwa uaminifu huu na miaka hii yote tumekaa pamoja kutatua changamoto nyingi ngumu, kuna wakati uliniona nimeshindwa kupata suluhisho? Sijawahi kushindwa na changamoto.
"Hata katika hali ngumu tuliyopitia au tutakayopitia siku za usoni, uaminifu ndio sababu ya yote. Kuaminiana kunanifanya nijiamini kwa pamoja, hakuna changamoto ambayo hatutashinda.”