NA LYDIA CHURI
JSC
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga amesema atafanya jitihada kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wanapata elimu kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama na kuzitumia kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Mahakimu.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Mkoa wa Manyara aliyasema hayo jana tarehe 1 Julai, 2024 wakati wa utoaji wa elimu kwa wajumbe wa Kamati ngazi ya mkoa kuhusu Kanuni na Mwongozo wa uendeshaji wa Kamati hizo yanayotolewa na Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama katika mikoa ya Manyara na Arusha.
‘Naishukuru Tume kwa kuona umuhimu wa kupita kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa na kutoa elimu kuhusu uwepo wa kamati zinazopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama,” alisema.
Alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, Mkoa wa Manyara utahakikisha vikao vya kamati za maadili vinakutana kama ilivyopangwa na vinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema wananchi wengi wa Mkoa wa Manyara hawana elimu ya kutosha kuhusu uwepo wa kamati zinazopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Mahakimu, hivyo mkoa utalibeba suala hili kama ajenda yake na kuwaelimisha wananchi.
“Tutapeleka elimu kila mahali katika mkoa wetu ili wananchi wafahamu ni wapi watakwenda kuwasilisha malalamiko yao pale wanapoona hawajatendewa haki hususan kwenye suala la maadili ya Mahakimu,” alisisitiza.
Akizungumzia nidhamu kwa Mahakimu, Mkuu wa Mkoa alisema Hakimu kufikishwa kwenye kamati ya maadili kwa kushindwa kusimamia kiapo chake siyo jambo jema, ni fedheha kwake na pia anauaibisha Mhimili wa Mahakama. Alisema Mahakimu hawana budi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi wa kazi yao.
Alisema kazi inayofanywa na Sekretariet ya Tume ya kuziimarisha Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya ni nzuri kwa kuwa itasaidia wananchi kupata haki zao kwani haki ni ustawi wa amani na utulivu na inachangia katika maendeleo ya nchi na ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya ametoa wito kwa wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Mkoa kuhakikisha wanakutana na kufanya vikao vya kamati vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria.
Alisema pamoja na kutoa elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili za Miko ana Wilaya, Watumishi wa Sekretariet ya Tume wamefika mkoani Manyara kwa lengo la kuzihuisha Kamati hizo na kuanzisha ushirikiano kati yake na wajumbe wa Kamati hizo ili ziweze kufanya kazi zake ipasavyo.
Alisema, ili kuhakikisha wajumbe wa Kamati za Maadili wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wajumbe hao katika ngazi ya Mkoa na Wilaya hawana budi kusoma, kuelewa na kuzitumia Kanuni za Maadili pamoja na Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati hizo uliotolewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Watumishi wa Sekratariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na kazi ya utoaji wa Elimu kwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya katika mikoa ya Manyara na Arusha pamoja na wilaya zake.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na.4 Sura ya 237.