Sekta ya Madini Tanzania inaendeshwa kwa uwazi-TEITI

DAR-Kaimu Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Mariam Mgaya ameeleza kuwa Sekta ya Madini nchini Tanzania inaendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji ili kutimiza matakwa ya Kimataifa ya uwazi na uwajibikaji (EITI Standard, 2023).
Ameyasema hayo leo Julai 10, 2024 alipotembelea banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, kwenye ripoti ya 14 ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 iliyowekwa wazi mwezi Juni, 2024 ni utekelezaji wa matakwa hayo ya Umoja wa Kimataifa wa EITI ambapo imelinganisha malipo ya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia na mapato ya serikali.
“Kupitia ripoti hiyo, utaona kwamba Kampuni kama North Mara Gold Mine Limited na Geita Gold Mining Limited zinachangia kwa kiwango kikubwa kwenye mapato ya serikali, zikichangia asilimia 40.89 na 19.94 mtawalia, kwa ujumla, sekta ya madini ilichangia asilimia 80.21 ya Mapato yote ya Serikali yatokanayo na Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa Mwaka wa Fedha 2021/22,” amesema Mariam.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo wa TEITI, Mgaya ameongeza kuwa, dhamira ya Tanzania ni kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia hatua ambayo inalenga kupunguza mianya ya rushwa, ukiritimba na ubadhirifu wa mali za umma.

Amesisitiza kuwa, ripoti za TEITI zipo wazi kwa matumizi ya umma na zinapatikana katika tovuti ya TEITI www.teiti.go.tz . Hivyo ni fursa kwa wananchi kupata taarifa rasmi ya rasilimali zako na kutoa maoni mahususi ili kuboresha sekta na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali zao hapa nchi.
Ripoti ya TEITI iliyozinduliwa Juni 29, 2024 pia inaeleza kuhusu mchango wa Kampuni za Mafuta na Gesi Asilia, pamoja na Kampuni zinazotoa huduma kwenye Sekta ya Uziduaji. Kampuni za Mafuta na Gesi zilikadiriwa kuchangia asilimia 17.02 ya Mapato ya Serikali yatokanayo na Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia.
Kwa ujumla, uwazi na uwajibikaji katika sekta ya madini ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi na kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinainufaisha taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news