Serikali imeweka mkazo kwenye rasilimali watu Sekta ya Afya-Lusajo

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Msaidizi wa Mipango na Bajeti wa Wizara ya Afya,Bw. Lusajo Ndagile amesema, Serikali imewekeza vya kutosha katika miundombinu ya afya ambapo kwa sasa inaendelea kutilia mkazo kwa upande wa changamoto ya rasilimali watu ili kuifanya sekta hiyo kuwa imara kwa ustawi bora wa jamii na taifa kwa ujumla.

"Kadri Serikali inavyoendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya ndivyo uhitaji wa rasilimali watu unakuwa mkubwa. Ndiyo maana tumebadili mwelekeo wa kuendelea kutoa mafunzo zaidi kwa wataalam wa afya katika ngazi mbalimbali.

"Na Serikali imeendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watumishi wengi wa afya wanapatikana. Tunatarajia pia mwaka huu kupata kibali cha ajira zaidi kwa ajili ya kuongeza rasilimali watu katika sekta ya afya nchini;
Amesema hayo leo Julai 29, 2024 wakati wa Kongamano la Kumbukizi la Rais mstaafu hayati Benjamin William Mkapa linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam.

"Wizara ina jukwaa pana katika sekta nzima, ni jukwaa ambalo linawaleta pamoja washirika mbalimbali ili kujadili changamoto za sasa za huduma za afya na kutafuta masuluhisho kwa pamoja.

"Hatua hii inasaidia Serikali kupata mawazo zaidi ikiwemo ufadhili endelevu katika afya, mfano bima mpya ya afya kwa wote.”

Pia, amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote umekusudia kuwapa nafuu wananchi wote bila kujali vipato vyao ili waweze kupata huduma bora za afya nchini.

Aidha, Lusajo amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo bekta binafsi ili kuhakikisha changamoto zilizopo hususani upande wa rasilimali watu zinapata ufumbuzi wa kudumu.

Katika mjadala ambao uliangazia Mipango ya Kuimarisha Ushirikiano wa Kimataifa na Mifumo ya Afya wawakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea Kusini, Canada na Indonesia waligusia namna ambavyo wenzetu wamepiga hatua katika upande wa afya.

Aidha, imeonekana Bima ya Afya kwa Wote ni mkombozi mkubwa si tu kwa kundi la watu wenye vipato vya juu bali wale wa vipato vya chini na kati.

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mheshimiwa Togolani Mavura amesema,utekelezaji wa bima umewezesha kuondoa mipaka baina ya vituo vya afya vya Serikali na vile binafsi.

"Bima ya afya ya kwao (National Health Insurance Service-NHIS) Korea Kusini inahudumia watu wote na katika watu inayowahudumia asilimia 78 wanakwenda kwenye vituo binafsi ni asilia 28 tu ndio wanaokwenda kwenye vituo vya Serikali."

Naye Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Indonesia, Mheshimiwa Makocha Tembele amesema,licha ya Taifa hilo kuwa na raia zaidi ya mara nne ya Watanzania wote wamepiga hatua kubwa katika sekta ya afya.

Amesema, Waindonesia licha ya kutoa bima ya afya kwa watu zaidi ya milioni 200, wao wapo kidijitali zaidi kwani mfumo wao wa afya upo kisasa.

Kupitia mfumo huo, wakati mwingine hauna sababu ya kufika kituo au hospitalini badala yake unaingia kwenye mfumo unaongea na Daktari kwa usaidizi wa haraka,bila usumbufu.

"Kwa hiyo asilimia 81 nchini indonesia wana bima ya afya na hii wameanza mwaka 2014."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news