Serikali kuokoa shilingi bilioni 2 za majenereta kila mwezi Katavi

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali inatarajia kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 2 kila mwezi ambazo huwa zinatumika kugharamia majenereta yanayowezesha kuwasha umeme mkoani Katavi.
Ameyasema hayo leo Julai 13,2024 wakati akisalimiana na wananchi wa Inyonga mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne mkoani Katavi.

Ni muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme wa Gridi ya Taifa kilichopo Inyonga mkoani Katavi ambayo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.

Rais Dkt.Samia amesema, kituo hicho kilichopo Wilaya ya Mlele eneo la Inyonga kitakua na uwezo wa kupokea na kupoza umeme ndani ya Mkoa wa Katavi.

"Na ndani ya wilaya hii, lakini kupeleka kwenye vituo vingine ambavyo vitawasha umeme ndani ya mkoa huu wa Katavi. Kama mnavyojua umeme ni tegemeo kubwa la uchumi wetu binafsi,lakini uchumi wa viwanda. Uchumi mkubwa.

"Na ndiyo maana katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 tuliahidi kuhakikisha kuwa nchi inazalisha umeme wa kutosha ili kukidhi mahitaji ya kiuchumi.

"Na tuliahidi kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote na maeneo ya pembezoni. Ninashukuru kwamba mkuu wa mkoa amesema kazi hii inaendelea vizuri.
"Ni kwa msingi huo sasa, nimekuja hapa kwenye ziara ya kikazi kukagua Mradi wa Kituo cha Kupooza Umeme cha Inyonga.

"Lakini, nimeona nikiwa pale kazi nzuri sanaaa..iliyofanyika na kwamba mwezi wa tisa mkoa huu, wilaya hii utatumia umeme wa Gridi ya Taifa.

"Tunakwenda kuachana na majenereta. Majenereta ambayo yanatumia pesa nyingi sana kama bilioni mbili kila mwezi kwa kuendesha majenereta na kuwasha umeme ndani ya Mkoa wa Katavi.

"Sasa tunakwenda kuachana na hayo na sasa tunakwenda kutumia Gridi ya Taifa. Lakini mbali ba ujenzi wa kituo kile nimeoneshwa pia jinsi TANESCO wanavyofanya kazi ya kujenga laini ambazo zitapokea umeme kutoka Kituo Kikuu Ubungo, lakini pia kusambaza umeme ule katika maeneo mengine.

"Na katika kazi ile vituo vitatu vinajengwa kuna hicho kituo cha Inyonga, lakini chenye kitapokea kutoka Sikonge na Inyoga itapeleka Mpanda."

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, vituo vitatu vya aina hiyo vinajengwa na mradi huo thamani yake ni shilingi bilioni 48.

"Kwa hiyo bilioni 48 zimetoka serikalini, tumezitumia kuhakikisha mkoa huu unapata umeme wa kutosha.
"Lakini mradi huu unaendana sambamba na mradi kama nilivyosema wa njia za umeme ambao ule mradi wa njia za kupokea na kupelekea umeme gharama yake ni shilingi bilioni 116.

"Hizo ni pesa nyingi sana ndugu zangu kwa hiyo niwaombe sana wana Katavi tutunze mradi huu."

Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani humo ambapo atakagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news