Serikali yaahidi kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na Jeshi la Magereza wilayani Ngara

KAGERA-Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepokea malalamiko ya mgogoro wa Ardhi kati ya Wananchi na Jeshi la Magereza katika Kijiji cha Rusumo Wilayani Ngara Mkoani Kagera.
Kauli hiyo imetolewa Julai 30, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo wakati akizungumza na Wananchi wa kata ya Rusumo Wilayani Ngara Mkoani Kagera baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kutazama mgogoro uliopo baina ya wananchi na Jeshi la Magereza.
Mhe. Sillo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nisikivu hivyo suala hilo la mgogoro huo atalifikisha katika vikao vya kamati ya maamuzi ili liweze kutatuliwa.

“Niwaombe wakazi wa kata na Kijiji hiki cha Rusumo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda sana na sisi kama Wizara tumewekwa kwa ajili ya kumuwakilisha yeye ili kutatua changamoto zenu, suala hili la Mgogoro huu nimelichukua na tutalishughulikia,”amesema Mhe. Sillo.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbunge wa Jimbo la Ngara Mhe. Ndaisaba Ruhoro amesema kuwa, mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya miaka 18 na kwamba umekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli za uzalishaji mali.

“Mhe. Naibu Waziri Mgogoro huu umedumu kwa zaidi ya miaka 18 sasa nikuombe utusaidie kwani wananchi wanakumbana na changamoto mbalimbali nakushindwa kufanya shughuli zao za uzalishaji mali ili kujiinua kiuchumi,”amesema Ruhoro.
Katika hatua nyingine Mhe. Sillo amesema Serikali ya Tanzania imetenga Dola milioni 100 kwa ajili ya kununua magari ya Zimamoto na Uokoaji hapa nchini ilikukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea.

“Eneo hili la Kituo cha forodha cha mpaka wa Rusumo ni eneo muhimu kwa ajili ya Uchumi wa Taifa letu na linahudumia nchini jirani ya Rwanda hivyo ni muhimu kuwa na vifaa vya utayari kwa ajili ya uokoaji pindi majanga yanapotokea,”amesema Mhe. Sillo.
Kauli hiyo ameitoa baada ya kutembelea Kituo cha forodha cha mpaka wa Rusumo na kuambiwa na Mbunge wa Jimbo la Ngara Mhe. Ndaisaba kuwa katika eneo hilo kumekuwa kukitokea ajali za Malori kuwaka moto lakini hakuna gari la Zimamoto pamoja na vifaa vya uokoaji.

“Mhe. Naibu Waziri hapa katika eneo hili la Rusumo kuna mitelemko mikali na miinuko kama ulivyo jionea mwenyewe na kila baada ya siku tatu kumekuwa kukitokea ajali za magari kuanguka wakati mwingine kuwaka moto hivyo kutokuwa na gari la Zimamoto na vifaa vya uokoaji tunalazimika kuomba kwa jirani zetu,”amesema Ruhoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news