NA GODFREY NNKO
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Mheshimwa Ummy Hamis Nderiananga amezindua rasmi Nyaraka za Usimamizi wa Maafa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 23,2024 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mkoani humo.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Nderiananga ametoa wito kwa wahusika kuhakikisha nyaraka hizo zilizoandaliwa zinakuwa chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau.
Pia, kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji tahadhari ya awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na maafa na kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa.
"Kwa niaba ya Serikali, naomba kutoa shukurani zangu za dhati kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili ambao umewezesha kuchangia jitihada za Serikali katika kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti.
"Aidha, niwapongeze Wilaya ya Kibiti kwa kutambua umuhimu wa kuandaa nyaraka hizi, kusimamia na kushiriki katika hatua zote za maandalizi ya nyaraka husika.
Mheshimiwa Nderiananga amesema, Tanzania imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii.
Amesema, maafa hayo yamekuwa yakisabibisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira.
Kutokana na changamoto hiyo, Mheshimiwa Nderiananga amesema,Serikali inasimamia na kuratibu shughuli za kuzuia na kukabiliana na majanga yakiwemo yale yanayovuka mipaka ya nchi kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na 6 ya Mwaka 2022.
Sambamba na kanuni zake za mwaka 2022 kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa inayotekeleza majukumu yake chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
"Suala la kuzuia na kukabiliana na majanga ni mtambuka ambalo linahitaji nguvu za pamoja katika kulishughulikia.
"Hivyo, hapa leo suala hili, linajidhihirisha wazi kwa kuona washiriki walioko hapa kutoka katika idara mbalimbali, taasisi za Serikali za Wilaya ya Kibiti na taasisi zisizo za kiserikali.
"Hawa wote ni wadau muhimu sana katika kushughulikia usimamizi wa maafa hapa wilayani Kibiti."
Amesema, moja ya majukumu ya Idara ya Menejimenti ya Maafa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 ni kutayarisha, kuhuisha na kuratibu utekelezaji wa sera, mipango, sheria, kanuni, mikakati na taratibu za utendaji kwenye shughuli zote zinazohusiana na usimamizi wa maafa Tanzania Bara.
Vile vile amesema, kazi ya uandaaji wa mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa na Mkakati wa Kupunguza Viatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti ni muendelezo wa utekelezaji wa jukumu hilo la msingi la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo limelenga kuimarisha usimamizi na uratibu wa maafa katika ngazi za mikoa na wilaya.
"Kama mnavyofahamu katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei, 2024 mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha maafa ya mafuriko katika maeneo mengi ikiwemo Mkoa wa Pwani.
"Mafuriko haya yalisababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira."
Amesema,kufuatia hali hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau ilichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuratibu upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika.
Pia,kuimarisha huduma za afya, kutoa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia na kijamii, kuratibu na kutekeleza operesheni ya utafutaji na uokoaji, kutafuta, kukusanya na kugawa misaada ya kibinadamu na kurejesha miundombinu iliyoathirika.
"Wote tunashuhudia namna ambavyo maafa haya yamekuwa yakisababisha matokeo hasi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Wilaya ya Kibiti kutokana na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu.
"Na hivyo, kuzorotesha hatua za maendeleo ambazo zilikuwa zimeishafikiwa katika eneo husika.
"Kwa kuzingatia hilo, Serikali kwa kushirikiana na UNDP imeandaa na kutekeleza Mpango Mahususi wa Kuijengea uwezo Wilaya ya Kibiti katika kuzuia, kupunguza madhara, Kujiandaa, kukabili na kurejesha hali endapo maafa yatatokea."
"Mpango huo ulihusisha kutoa elimu kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Rufiji, kufanyika kwa tathmini ya kubaini vihatarishi vya maafa, uwezekano wa kuathirika na uwezo wa jamii kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa.
"Ikiwemo kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana Maafa pamoja na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti."