SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri

NA LWAGA MWAMBANDE

INAKADIRIWA zaidi ya abiria 1,000 leo Julai 25,2024 wamesafiri kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kupitia treni ya abiria ya umeme ya SGR.
Picha kwa hisani ya Milardayo.

Ni kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kuahidi safari hizo zitaanza mwezi huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa ni miongoni mwa waliosafiri na treni hiyo leo ambapo amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwezesha kukamilika kwa reli na safari hizo kuanza.

Kadogosa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili jijini Dodoma kwa treni hiyo amesema,hatua hiyo ni utekelezaji wa maeelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo mwaka jana kuwa ifikapo mwezi Julai, mwaka huu lazima usafiri wa treni ya umeme kutoka Dar es Saalam kuja Dodoma uwe umeshaanza rasmi.

“Leo tumetoka Dar majira ya 12 asubuhi na kufika Dodoma majira ya saa nne asubuhi na hii ni kutokana na kuwa kuna eneo tulisimama sana kwa ajili ya kupishana na treni iliyotoka huku, lakini kadri siku zinavyokwenda tutaendelea kuboresha changamoto ambazo zimejitokeza leo kama ilivyokuwa wakati tulivyoanza safari za Dar hadi Morogoro.”

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, haya ni mageuzi makubwa yenye kuleta matokeo chanya si tu kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji nchini bali kuwezesha kuharakisha shughuli za maendeleo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla. Endelea;

1. Mengine tunyamazie, ila mengine tuseme,
Vipi tulinyamazie, kubwa hivi tusiseme?
Tuache tumpashie, kelele zote zizime,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

2. Tokea kwa Magufuli, mradi usisimame,
Tena mradi aghali, funga mkanda tukome,
Sasa Dare siyo mbali, wengine namba wasome,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

3. Wale wameshasafiri, Moro na Dar waseme,
Usafiri ni mzuri, mzuri sana wazime,
Hata jinsi wafikiri, kama Uchina safari,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

4. Amethibitisha Mama, hili acha tumseme,
Kazi hazitasimama, taendeleza alime,
Tunaona tunasoma, na kwenye gari tuzame,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

5. Na jinsi kazi ilivyo, bora sasa msiseme,
Kazi yenda hivyohivyo, acha watu wajitume,
Lakini sasa ilivyo, hebu tuache tuseme,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

6. Treni ya mwendokasi, kwa heshima tusimame,
Ni kweli siyo tetesi, Serikali tuipime,
Jinsi yafanya kwa kasi, wabishibishi wakome,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

7. Miradi hii miwili, mikubwa heri tuchume,
Umeme na hii reli, Serikali tutazame,
Itatufikisha mbali, nasi kazi tujitume,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

8. Serikali ya Samia, hebu acha tuiseme,
Imetuthibitishia, matunda haya tuchume,
Wengi tunafurahia, acha TZ ivume,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

9. La muhimu kwetu sote, kuituza tusikome,
Tuwe ni walinzi wote, wahalifu tuwachome,
Reli kwa miaka yote, iwe bora tuitume,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

10. Maendeleo zaidi, wananchi tujitume,
Kufanya kazi zaidi, na kodi zetu zisome,
Yafanywe mema zaidi, matunda yake tuchume,
SGR Dodoma, mwendelezo ni mzuri.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news