Sheria imetupa uwezo wa kutoa mkopo wa muda mfupi kwa Serikali-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa,Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 Sura ya 197 imewapa uwezo wa kuikopesha Serikali mkopo wa muda mfupi ili iweze kuziba pengo la muda mfupi na si kufadhili bajeti.
Hayo yamesemwa leo Julai 22,2024 na Agathon Kipandula, Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

"Benki Kuu ipo kwa mujibu wa Sheria ya Kuanzishwa Kwake Sura ya 197. Sheria tunayoitumia sasa ni Sheria ya Mwaka 2006.

"Benki Kuu ni benki ya Serikali na mashirika ya umma, kwa hiyo fedha zote za Serikali na mashirika au taasisi za umma kwa Serikali zote mbili (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) zinatunzwa Benki Kuu.

"Lakini pia, sheria kwa sababu ya kuwa na mteja ambaye ni Serikali, sheria hiyo pia imeweka au imetoa nafasi ya kutoa mkopo wa muda mfupi kwa Serikali.

"Mkopo huo kwa mujibu wa sheria unaitwa advance ambao kwa mujibu wa sheria unatolewa kwa Serikali ili kurekebisha kushuka na kupanda kwa mapato ya Serikali. Kwa hiyo hicho kipengele ndiyo kinafanya sasa Benki Kuu kwa muda mfupi ndiyo inakopesha Serikali."

Kipandula amesema,kwa mujibu wa sheria hiyo umewekwa ukomo wa mkopo ambao ni asilimia 18 ya mapato ya mwaka jana ambao utadumu ndani ya siku 180.

"Kwa hiyo kuna sheria ambayo inatusimamia katika kuendesha shughuli za Serikali ikiwemo kutoa huduma ya mkopo wa muda mfupi kuziba pengo au kuziba nakisi ya muda mfupi.

"Mkopo huo sio ule ambao tuna-determine amount kwamba watakopa kiasi hiki, huu unabalance cash flow yake kwamba kama leo anajukumu la kulipa shilingi 10,000 na alizo nazo ni shilingi 5,000 basi shilingi 10,000 itakuja kama overdraft na akipata fedha zake basi atarudisha.’’

Vile vile,amesisitiza kuwa si kweli kwamba Serikali ilikopeshwa kiasi cha fedha na BoT kwa aina tofauti, kwani hata kwenye vitabu vya Serikali hakuna kiasi hicho.

Aidha, amesema kuwa mkopo wa aina hiyo hauhitaji kupitishwa na Bunge isipokuwa wataonesha kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hata hivyo, amesema sheria hiyo ya kuikopesha Serikali mkopo wa muda mfupi ipo kwa benki kuu nyingi duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news