Shilingi bilioni 33 kukarabati Meli ya MV Liemba

KIGOMA-Kampuni ya M/S Brodosplit JSC ya Nchini Croatia kwa kushirikiana na Kampuni ya kizalendo ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG) wamekabidhiwa rasmi meli kongwe ya MV. Liemba ambayo ni maalumu kwa abiria na mizigo iliyopo mkoani Kigoma (Ziwa Tanganyika) ili waanze mara moja ukarabati wa viwango ambao utachukua takribani miaka miwili.
Wakandarasi wa Meli ya MV Liemba wakikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma mjini, Salum Kalli (Kushoto) zawadi ya saa yenye picha ya meli hiyo kama kumbukumbu ya mwisho kabla ya kuanza kwa ukarabati mkubwa ambao utaenda kuubadilisha kabisa muonekano wa meli ya MV Liemba baada ya kukamilika kwa ukarabati huo. (Picha na Mpiga Picha Wetu).

Akizungumza jana mkoani Kigoma mara baada ya makabidhiano, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG), Rayton Kwembe amesema kuwa ukarabati wa meli hiyo kongwe ya abiria na mizigo ya MV. Liemba utatumia gharama ya shilingi bilioni 33.

Amesisitiza watajitahidi kufanya kazi kwa wakati na weredi wakishirikiana na mkandarasi mkuu ambaye ni Kampuni ya M/S Brodosplit JSC ili kwenda sambamba na muda uliopangwa kwenye mkataba.
Meneja wa Mradi wa ukarabati wa meli kongwe ya MV. Liemba (Upande wa Serikali) Mhandisi Elias John Kivara (mbele) akiwa katika kikao kazi na wakandarasi wanaofanya ukarabati wa meli hiyo kutoka kampuni ya DMG na M/S Brodosplit JSC ya Nchini Croatia kabla ya makabidhiano ya meli hiyo Mkoani Kigoma jana.

“Tunaahidi ukarabati uliotukuka na wenye viwango ambapo kwenye utekelezaji huu tunafanya kwa ushirikiano na Kampuni ya M/S Brodosplit JSC ya Nchini Croatia ambao ndiyo wakandarasi wakuu kwenye mradi huu wenye gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 33.
“Tunaishukuru sana serikali yetu ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini na tunaiahidi Serikali kuwa kamwe hatutawaangusha katika utekelezaji wa mradi huu.

“Tutajitaidi kwa hali na mali kuhakikisha kuwa mradi huu wa ukarabati tunaufanya kwa muda muafaka ili meli hii ambayo ni maalumu kwa usafirishaji wa mizigo na abiria iendelee kufungua fursa nyingi za ajira binafsi na kupunguza gharama za usafirishaji sambamba na kuongeza tija katika shughuli za biashara na hivyo kuwafanya wananchi kunufaika.”

Mkurugenzi huyo wa DMG alidokeza kuwa kampuni yao ina uzoefu wa muda mrefu na utaalam wa kushiriki katika miradi mikubwa inayohusisha matengenezo ya meli na uundaji kwa ujumla kutoka hatua ya awali mpaka kukamilika.

Alibainisha: “Lakini pia Kampuni yetu ya DMG ipo katika mahusiano mazuri na taasisi za fedha ambapo mahusiano haya yanatusaidia kupata fedha stahiki kwa wakati pale zinapoitajika ili kusaidia miradi yetu kwenda na muda ulipangwa."alisema.
Meneja wa Mradi wa ukarabati wa meli kongwe ya MV. Liemba (Upande wa Serikali) Mhandisi Elias Kivara (kulia ) akishikana mikono na Dongmyung Kwak, meneja mradi kutoka upande wa wakandarasi wanaofanya ukarabati wa meli hiyo wakati wa makabidhiano ya meli hiyo Mkoani Kigoma jana.

Ili kutekeleza vyema miradi ya ujenzi wa meli na matengenezo yake, DMG ilianzisha Idara ya kushughulikia mambo hayo mwanzoni mwaka 2017 kwa nia ya kutatua changamoto zinazoikabili Sekta hii iliyo katika uchumi wa bluu kwa kuleta maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amewataka wakandalasi wa mradi huo wa ukarabati wa meli hiyo kukamilisha kazi waliyopewa kwa wakati kama ambavyo imebainishwa kwenye mkataba wa makubaliano.

“Cha msingi ni kuendana na matakwa ya mkataba hakika ilikuwa ni ndoto lakini sasa imetimia, watu wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla wana furaha kusikia habari hii kuwa sasa ukarabati wa meli hii unaanza rasmi,” alisema DC Kalli.

Allen Mtembelo, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (Mscl), amesema: “Wakandarasi tayali wapo site na wapo tayari kuanza mradi huu wa ukarabati wa Mv Liemba.”

Serikali iliamua kuwekeza katika ukarabati wa meli hiyo kutokana na uimara wake na kuokoa gharama ya kujenga au kutengeneza meli mpya.
Meneja wa Mradi wa ukarabati wa meli kongwe ya MV. Liemba Mhandisi Elias Kivara (wa nne kutoka kulia ) akiwa katika picha ya pamoja na wakandarasi ambao wanafanya ukarabati wa meli hiyo kutoka kampuni ya DMG na M/S Brodosplit JSC ya Nchini Croatia wakati wa makabidhiano ya meli hiyo Mkoani Kigoma jana.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya meli hiyo Meneja wa Mradi huo Mhandisi Luteni Kanali Elias John Kivala amesema: “Kwa niaba ya serikali, tunawaomba wakamilishe mradi huu kwa muda muafaka, na tunawaomba wafanye fast track (haraka zaidi), kama serikali tunawaahidi kuwapa ruhusa ya kufanya kazi kwa masaa 24.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news