MANYARA-Zaidi ya shilingi milioni 115 zitatumika kujenga Kituo cha kisasa cha Polisi katika Kijiji cha Bashnet Wilayani Babati ili kukidhi haja ya kusogeza Huduma za kipolisi kwa Wananchi.
Hayo yamesemwa Julai 23, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mhe. Daniel Sillo, katika muendelezo wa ziara yake ya Kiserikali ya Kijiji kwa Kijiji, Kata kwa Kata, Kitongoji kwa Kitongoji katika Jimbo la Babati Vijijini akisikiliza na kutatua kero mbalimbali za Wananchi.
Mhe. Sillo amesema Kituo hicho kitajengwa katika eneo ambalo Serikali ya Kijiji itatenga.
Ombi hilo la Wananchi wa Kijiji hicho kupatiwa Kituo cha Polisi limekuja kutokana na ukweli kwamba Kijiji cha Bashnet kinakua kwa kasi hivyo upo uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa matukio ya kihalifu sambamba na kufuata Huduma hiyo kwa umbali mrefu.
Katika ziara hiyo Mhe. Sillo ameambatana na wataalam mbalimbali kutoka sekta ya elimu, afya, miundombinu na nishati ili kutoa ufafanuzi na majibu ya hoja mbalimbali za wananchi.
Pia katika ziara yake Mhe. Sillo ameambatana na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Jackson Hhaibey.