DODOMA-Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo ameonesha kutofurahishwa na kiwango kidogo cha watanzania kutumia mbolea ya Kiwanda ya cha Intracom kilichopo Nala jijini Dodoma ambacho kimetokana na matunda ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa nchini Burundi.


Dkt. Jafo ameongeza kwa "Sijafurahishwa na mwenendo huu, tunafanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo Rais ameongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh.Bilioni 294 hadi Sh.Trilioni 1.2 ni wazi Rais ana matamanio makubwa sana, niwaombe watanzania kutumia mbolea ya kiwanda hichi,"amesema.
Amebainisha kuwa, kiwanda hicho kwasasa tayari uwekezaji wake ni zaidi ya Sh.Bilioni 500 na ujenzi bado unaendelea maeneo mengine na inatarajiwa uwekezaji uwe zaidi ya shilingi trilioni moja.
"Kiwanda kwa sasa kina waajiriwa 907 na zaidi ya 600 ni watanzania, na kitakapokamilika uwezo wake ni kuajiri watu 3000 hadi 4000, haiwezekani mbolea izalishwe hapa isinunuliwe Tanzania, hii ni kumkwamisha Rais, kwa nini tununue mbolea maeneo mengine nje ya nchi, lakini tushindwe kununua hapa nchini.
"Mimi Waziri wa Viwanda sitakubali hata kidogo kuona viwanda vinavyojengwa Tanzania vinashindwa kuwezeshwa kufanya kazi yake hii kubwa, sisi kama Serikali tutajadiliana namna ya kufanya ili viwanda vinavyojengwa nchini vifanye kazi vizuri,"amesema.
Amewahakikishia wawekezaji kuwa atasimamia kuhakikisha viwanda vilivyowekezwa nchini vinakidhi matarajio ya Rais.
"Tutavilinda viwanda vyetu hapa nchini vifanye kazi vizuri na vijana wetu wapate ajira na dhamira ya Rais Samia ya kuhangaika kutafuta wawekezaji lazima itimie,"amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Kiufundi wa Kiwanda hicho, Mhandisi Victor Ngendazi, amesema kiwanda hicho kilianza kujengwa Julai 2021 na lengo lilikuwa kutengeneza mbolea tani 600,000 lakini kutokana na maombi ya serikali ya Tanzania wameongeza hadi tani milioni moja.

Amesema,wamekuwa wakishirikiana na serikali kutatua changamoto zilizokuwapo zikiwakabili na kusisitiza uwezo wa uzalishaji upo wa kutosha.

Amesema uwezo wa Kiwanda ni mkubwa na kama wataendelea kukosa soko watasimamisha uzalishaji.