*Ni sekondari ya wasichana ya Lugalo ya Mkoa wa Iringa
*Amsimamisha kazi Mhandisi, aagiza Afisa Elimu apewe onyo
IRINGA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Iringa na kuagiza Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Emmanuel Sigachuma asimamishwe kazi mara moja.
Pia ameagiza Afisa Elimu ngazi ya Sekondari ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Nelson Milanzi apewe onyo kwa kushindwa kusimamia matumizi ya fedha za ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Lugalo iliyoko kata ya Mbigili, wilayani Kilolo.
Pia ameagiza Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu, Lain Ephraim Kamendu aitwe ili ahojiwe pamoja na wenzakekuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo. Yeye alistaafu Aprili, mwaka huu na ujanzi ulianza yangu Agosti, 2023.
Amefikia uamuzi huo leo Jumatatu, Julai 8, 2024 baada ya kukagua ujenzi wa sekondari hiyo na kukuta kasoro nyingi kwenye madawati, vyumba vya maabara na bwalo la wanafunzi ilhali walishapewa sh. bilioni tatu za kukamilisha majengo yote ya shule hiyo.
Kasoro kubwa zilizobainika ni ukosefu wa nyavu za kuzuia mbu kwenye baadhi ya madirisha wakati mkandarasi ameshalipwa fedha yote, viti na meza za wanafunzi kupasuka wakati havijaanza kutumika.
Viti hivyo vilikabidhiwa tangu Desemba, 2023 na muda wa matazamio ulikuwa ni miezi sita lakini mkandarasi keshalipwa fedha zote.
Katika ukaguzi wa bwalo, Waziri Mkuu alielezwa na Mhandisi Sagachuma kwamba bwalo hilo lilitengewa sh. milioni 774 na wamekwishatumia sh. milioni 341 hadi kufikia hatua ya linta ambayo alidai ni sawa na asilimia 40 ya ujenzi wake.
Alipoulizwa fedha zilizobakia ziko wapi, Mhandisi huyo alijibu kwamba hazipo. Afisa Elimu Sekondari naye hakuweza kueleza ziko wapi au kama kuna vifaa vilivyokwishanunuliwa vimewekwa wapi.
"Unasema utajenga kwa chuma hapa juu, hizo nondo ziko wapi? Mabati yako wapi? Majiko yako wapi? Hapa tunatarajia kuwa na watoto 172, je watakula wapi hawa na masomo yameshaanza?" alihoji Waziri Mkuu bila kupatiwa majibu.
“Wewe ni Afisa Elimu na kazi yako ni kusimamia ujenzi wa shule zote, ni kwa nini hukutoa taarifa ya kusuasua kwa ujenzi kwenye Kamati ya Ulinzi ya Wilaya yako? Taarifa nilizonazo ni kwamba Mkurugenzi aliyekuwepo alikuwa anakupangia kazi kwenye vituo vya mbali ili usije hapa, lakini bado ulikuwa na wajibu wa kutoa taarifa juu ya mwenendo huo.”
Kwenye ujenzi wa maabara za shule hiyo, Waziri Mkuu amehoji ni kwa nini mifereji ya kupitisha gesi na maji machafu imezibwa yote.
“Mifereji haina vishikio, wamejaza matofali hata mwalimu akitaka kukagua mifumo ya gesi au mifereji ya maji machafu hawezi kuinua hilo tofali. Mifuniko ya mifereji inayopitisha maji, bomba za umeme na gesi kwenye maabara ya shule hiyo itolewe na irekebishwe upya,” ameagiza.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Joachim Nyingo asimamie zoezi la kurudisha madawati yaliyoletwa ambayo ni mabovu kwa gharama za mkandarasi ili yaletwe mengine mapya. Madawati (meza na viti vyake) mengi yalikuwa yamepasuka katikati au pembeni na yalikuwa yamepangwa darasani.
“Nimeagiza fundi aliyejenga madirisha atafutwe, aletwe ili aweke nyavu kwenye jengo la utawala. Aliyetengeneza madawati aitwe akayatengeneze upya madawati hayo kwa viwango vinavyotakiwa na kwa gharama zake.”
Pia amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU, Mkoa wa Iringa, awahoji watumishi hao na aanze uchunguzi mara moja.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekabidhi hati ya kiwanja chenye ukubwa wa ekari 50 kwa uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ili waweze kuanza ujenzi wa tawi la chuo hicho katika wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.