CAIRO-Mchezo wa kirafiki kati ya Simba SC dhidi ya Telecom FC uliopigwa Uwanja wa Mercure nchini Misri umemaliza kwa kupata ushindi wa mabao 2-1.
Kupitia mtanange huo wa leo Julai 28,2024 mpira ulianza kwa kasi huku timu zikishambuliana kwa zamu na kila moja ikionekana kutafuta bao la mapema,lakini safu za ushambuliaji zilipoteza umakini.
Dakika ya 18 wenyeji Telecom walipata bao la kuongoza lililofungwa kwa kichwa na Ashour Shika, aliyeunganisha mpira wa krosi.
Baada ya bao hilo,Simba SC waliendelea kufanya mashambulizi, lakini Telecom FC walikuwa makini huku wakicheza zaidi kwa kujilinda.
Kipindi cha pili Simba SC walirudi kwa kasi na kuongeza presha kwenye lango la Telecom FC ambapo dakika ya 62, Valentino Mashaka awapatia bao la kusawazisha baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Valentine Nouma.
Kocha Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya kuwatoa Freddy Michael, Augustine Okajepha, Ladaki Chasambi na kuwaingiza Awesu Awesu, Willy Onana na Valentino Mashaka.
Dakika ya 77 kocha Fadlu alifanya mabadiliko ya kumtoa mlinzi Valentine Nouma na kumuingiza tena Chasambi.
Chasambi aliwapatia Simba SC bao la pili dakika ya 88 kwa kufunga kwa tiktak baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Kelvin Kijili.
Hata hivyo, hadi dakika ya 90 inatamatika Simba SC kutoka jijini Dar es Salaam imeibuka kuwa wababe wa Telecom FC kwa ushindi huo ambao tunaweza kusema ni bao moja kwa bila.