Tanzania, Oman zajipanga kukuza biashara

MUSCAT-Ubalozi wa Tanzania nchini Oman umeandaa Kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika nchini Oman kuanzia tarehe 26 – 28 Septemba 2024.
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf.

Hayo yameelezwa wakati wa kikao kati ya Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf kilichofanyika Julai 15, 2024.

Katika mazungumzo hayo, wawili hao walisisitiza umuhimu wa kuanzisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Jumuiya ya Ushirikiano wa nchi za Ghuba (GCC) na Jumuiya za kikanda ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Balozi Fatma alisisitiza pia umuhimu wa Oman kushiriki maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam, maarufu Sabasaba yanayofanyika kila mwaka mwezi Julai.

Kwa upande wake, Waziri Qais aliafiki mapendekezo ya Oman kushiriki maonesho ya sabasaba ambapo aliahidi kuwa atatembelea Tanzania na wafanyabiashara wakubwa ili kujionea fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Alitoa mwaliko kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuzuru Oman kwa lengo la kujionea maendeleo ya viwanda, hasa eneo la viwanda la Sohar na kujadili namna ya kuanzisha makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara (MoU) baina ya pande mbili. Alipendekeza ziara hiyo kufanyika katikati ya mwezi wa Septemba au Oktoba 2024.
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf wakikabidhiana zawadi baada ya mazungumzo yao.

Viongozi hao walihimiza umuhimu wa usafiri wa moja kwa moja wa ndege ya mizigo kati ya Tanzania na Oman ili kurahisisha biashara. Kufuatia umuhimu huo, Balozi Fatma alieleza kuhusu kusainiwa kwa Mkataba mpya wa Ushirikiano wa Anga (BASA) baina ta Tanzania na Oman Julai 16, 2024 utakaoiwezesha Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania kufanya safari zake nchini Oman.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa viongozi hao kuhimiza umuhimu wa kusaini Mkataba wa Kuepuka utozaji wa Kodi mara mbili ili kutimiza azma ya kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news