DODOMA-Ujumbe wa watu sita kutoka nchini Marekani Julai 16, 2024 umekutana na Wataalam wa Wizara ya Madini na Taasisi zake na kujadiliana kuhusu ya fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini.

Katika majadiliano hayo, GST imewasilisha mada juu ya fursa zilizopo kupitia taarifa za tafiti mbalimbali zilizofanyika hapa nchini ambapo Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST Masota Magigita ameelezea kuhusu hali ya jiolojia ya Tanzania na uwepo wa madini kupitia tafiti zilizofanyika kwa njia ya Jiolojia , Jiofikia na Jiokemia.
Aidha, Magigita amefafanua kuwa katika taarifa za jiosayansi zilizopo zimebainisha aina mbalimbali za madini yakiwemo madini mkakati, madini ya metali, madini ya vito, madini ujenzi na madini adimu (REE).
Naye, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, Andrew Mgaya amesema kuwa Tanzania inaendelea na uzalishaji wa madini ya kinywe ambapo mwaka 2023/2024 kiasi cha tani 196,682.58 zilizalishwa kutoka tani 10,069.55 zilizozalishwa kwa mwaka wa 2022/2023.
