TEF yalaani mwandishi wa The Guardian kushambuliwa shuleni Ubungo

NA GODFREY NNKO

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeelezea kusikitishwa na kitendo cha kushambuliwa kwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya The Guardian, Dickson Ng’hily, kilichofanywa na walimu wa Shule ya Msingi Kwembe wilayani Ubungo, Dar es Salaam wakati akitelekeza majukumu yake.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 12, 2024 na Mwenyekiri wa TEF, Deodatous Balile ambapo amefafanua kuwa, shambulio hilo lilitokea Julai 10, 2024 kwa madai kuwa amewapiga picha wanafunzi wa shule hiyo wakisoma nje ya madarasa chini ya mti.

"Baada ya kumshambulia, walimu walikwenda mbali zaidi kwa kumpeleka mwandishi huyo katika ofisi za Serikali ya Mtaa na baadaye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.

"Licha ya kipigo, walimu hao na wanafunzi waliharibu vifaa vyake vya kazi ikiwemo simu ya mkononi waliyoipasua kioo, wakamnyang’anya na kufuta picha alizopiga.

"Tunaomba ifahamike kuwa uandishi wa habari chini ya Kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Huduma za Habari (MSA) ya Mwaka 2016 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2023, ni taaluma inayotambulika kama taaluma nyingine nchini.

"Tumeona utetezi wa Wilaya ya Ubungo wakisema, “aliwekwa chini ya ulinzi kujiridhisha kama ana kibali cha kupiga picha”.

"Utetezi huu ni mwendelezo wa jinai sawa na walivyofanya walimu waliompiga Ng’hily. Tunajiuliza ukaguzi huo walitaka kuufanya kwa kutumia sheria ipi au walipata wapi mamlaka hayo?.

"Nani kawambia mwandishi wa habari akikuta tukio linaendelea anapaswa kuandika barua ya maombi ya kibali cha kupiga picha, kiidhinishwe kwanza ndipo arudi kupiga picha? Hivi hilo tukio atalikuta likiendelea akifuata utaratibu huo?.

"Duniani kote, mwandishi akikuta tukio anapiga picha kwanza kisha anawatafuta wahusika kupata ufafanuzi. Kwa nini Wilaya ya Ubungo na Walimu wa Shule ya Msingi Kwembe wanataka kutunga kanuni mpya isiyokidhi vigezo vya uandishi wa habari?.

"Kitendo kilichofanywa na walimu hao ni jinai na hujuma dhidi ya juhudi anazofanya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kurejesha uhuru wa vyombo vya habari nchini kwa kuzuia waandishi kukamatwa, kupigwa, kuzuiwa kufanya kazi, kunyanyaswa na mengi ya aina hiyo ambayo ameyazuia tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021.

"Hali iliyoipandisha Tanzania katika viwango ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa nafasi 46, yaani kutoka nafasi ya 143 hadi nafasi ya 97.

"Vitendo vya aina hii vikiendelea nchi yetu itashuka tena na kuathiri kuaminika kwake mbele ya jamii ya kimataifa, hivyo kukimbiza wawekezaji.

"TEF tunalaani kwa nguvu zote kitendo hiki na tunavisihi vyombo vya dola vimpe ushirikiano wa kutosha Mwandishi Ng’hily, ambaye tayari ameanza mchakato wa kufungua kesi yajinai dhidi ya wote waliohusika katika kadhia hii.

TEF tutamuunga mkono hatua kwa hatuakuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kulipa gharama ya hasara waliyoisababisha na iwe fundisho kwa wengine waache kujichukulia sheria mkononi,"amefafanua kwa kina Mwenhyekiti wa TEF, Balile.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news