MBEYA-Wafanyabiashara wa mbolea nchini wametakiwa kushirikiana na serikali katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ya mbolea kwa wakulima.
Mgeni rasmi na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joshua Ng'ondya (katikati) na meza kuu wakiwa katika picha na watumishi wa TFRA walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Umoja wa Wauza Pembejeo wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini tarehe 25 Julai, 2024.
Wito huo umetolewa na Kaimu Meneja wa Mamalaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng'ondya akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Joel Laurent aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Mbolea wa Nyanda za Juu Kusini (SHAU) na Mkutano Mkuu wa wanachama wake uliofanyika katika ukumbi wa TUGHIMBE jijini Mbeya.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joshua Ng'ondya akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Umoja wa Wauza Pembejeo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (SHAU) tarehe 25 Julai, 2024 Jijini Mbeya.
Ng'ondya amesema, hivi karibuni mamlaka imezindua kampeni ya Kilimo ni Mbolea yenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea pamoja na usajili wa wakulima na kuwasihi wafanyabiashara hao kuwa miongoni mwa watekelezaji wa utoaji wa elimu ya mbolea kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na baadaye kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.
Aidha, amewataka wafanyabiashara hao kuwa waaminifu na waadilifu ili kuepuka mkono wa sheria na kueleza Serikali haitamfumbia macho yeyote atakayekiuka na kuuza mbolea za ruzuku kinyume na taratibu zilizowekwa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya Mohamed Aziz Fakihi akizungumza na wafanyabiashara wa pembejeo wa Nyanda za Juu kusini (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa umoja wao uliofanyika katika ukumbi wa TUGHIMBE jijini Mbeya tarehe 25 Julai, 2024.
Pamoja na hayo, Ng'ondya aliwataka mawakala hao kuwahamasisha wakulima kujisajili ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku na kwa upande wa wafanyabiashara amewataka kuonyana wao kwa wao pindi wanapomwona mmoja wao akikiuka taratibu ili kumwepusha na changamoto ya kuona biashara anayoifanya ni kero badala yake impe manufaa.
Alisema, lengo la kutoa ruzuku ya mbolea ni kuwasaidia wakulima waweze kupunguza gharama za uzalishaji na kuwafanya wakulima wazalishe kwa tija.
Dkt. Mshindo Msolla wa Kiwanda cha Madini na Mbolea Minjingu (MFFL) akipokea cheti baada ya kudhamini Mkutano wa Wana Umoja wa Wauza Pembejeo wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini tarehe 25 Julai, 2024 uliofanyika katika ukumbi wa TUGHIMBE jijini Mbeya.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya Mohamed Aziz Fakihi ameeleza kuwa, serikali inapenda kuona umoja huo unafanya vizuri ili kuwanufaisha wakulima kwa kuwafikishia pembejeo katika maeneo yao na kwa wakati unaofaa.
"Kilimo sio siasa, tunatarajia mtafanya kazi na sio siasa kwenye umoja wenu huu unaozinduliwa siku hii muhimu,"Fakihi alisisitiza.
Wana Umoja wa Wauza Pembejeo wa Nyanda za Juu Kusini wakifuatilia mada wakati wa hafla ya kuzindua umoja wao uliofanyika katika ukumbi wa TUGHIMBE Jijini Mbeya tarehe 25 Julai, 2024.
Mwisho amewaasa kushiriki kwenye uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa na kuwaomba kuchagua viongozi walio bora.