TGC mpya licha ya kwenda kulipendezesha Jiji la Arusha, heshima ya uongezaji thamani madini ya vito itapatikana hapa

ARUSHA-Wizara ya Madini imemkabidhi rasmi Mkandarasi Kampuni ya Ujenzi ya Skywards eneo litakapojengwa Jengo la Kisasa la Ghorofa Nane (8) la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Julai 17, 2024 jijini Arusha katika Kituo cha TGC na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Madini, Ashura Urassa kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mratibu wa Kituo hicho Ally Maganga, wataalam kutoka Wizara ya Madini na TGC, Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Arusha Mussa Shanyangi, pamoja na Mshauri Elekezi Kampuni ya Epitome Architects.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Mratibu wa Kituo hicho, Ally Maganga amesema kukamilika kwa jengo hilo kunatarajia kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Uongezaji Thamani Madini ya Vito na usonara na kueleza kwamba, TGC imejipanga kutoa elimu itakayokidhi viwango vya kimataifa kutokana na miundombinu muhimu inayotarajiwa kuwekwa katika jengo hilo ikiwemo ushirikiano ulioanzishwa na taasisi nyingine za kimataifa ambao umelenga kuzalisha watalaam wenye viwango vyenye ubora wa juu.

"Elimu itakayotolewa itakidhi viwango vya kimataifa na kituo hiki kinakwenda kuwa kitovu cha madini ya vito na mnyororo mzima wa shughuli za uongezaji thamani madini ya vito. Tunatarajia baada ya kukamilika watanzania watanufaika pamoja na kuwavutia wanafunzi zaidi kutoka nje ya Tanzania,’’ amesema Maganga.
Kituo cha TGC kinatoa mafunzo ya uongezaji thamani madini yakihusisha ukataji, ung"arishaji madini ya vito, utambuzi wa madini, jiolojia na huduma mbalimbali kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya vito. Aidha, tayari kituo hicho kimepokea wanafunzi kutoka nchi za Kongo na Afrika Kusini wanaoendelea na mafunzo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Wizara ya MadiniAshura Urassa, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini, amemtaka Mkandarasi kufanya kazi kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotolewa pamoja na muda uliowekwa kulingana na mkataba wa ujenzi ili kuepuka usumbufu na kutokukwamisha malengo ya Serikali ya ujenzi wa jengo hilo.

Naye, Mwakilishi wa kampuni ya ujenzi ya Skywards Mhandisi Innocent Shirima, ameishukuru Serikali kwa kuiamini na kuipatia kampuni hiyo ya wazawa kujenga jengo hilo na kueleza kwamba matarajio ya kampuni hiyo ni kufanya kazi kwa viwango vya juu kutokana na uzoefu wake.
Pia, Mtaalam Elekezi kutoka Kampuni ya Eptome David Kibebe amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza manufaa kwa Wizara katika shughuli za uongezaji thamani madini pamoja na kupendezesha mandhari ya jiji la Arusha na kueleza, ‘’tutakuwa bega kwa bega na Serikali kuhakikisha mradi huu unakamilika kama ulivyopangwa,’’.

Ujenzi wa Jengo la TGC ni miongoni mwa maeneo mengine ya kipaumbele ambayo Wizara imepanga kuyatekeleza katika Mwaka wa Fedha 2024/25 ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini ya vito.
Juni 26, 2024 jijini Dodoma, Wizara ilisaini Mkataba wa ujenzi wa jengo hilo na kampuni mbili za wazawa zilizoungana za Skywards na Lumocons. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 33.42 hadi kukamilika kwake.

#InvestInTanzaniaMiningSector
#Vision2030:MadininiMaisha&Utajiri

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news