DAR-Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeomba radhi kufuatia hitilafu ya umeme iliyojitokeza kati ya Stesheni ya Kilosa na Kidete ambayo imesababisha Treni ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) iliyokuwa inafanya safari zake kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea jijini Dodoma kusimama kwa muda wa saa mbili Julai 30,2024
Taarifa iliyotolewa na TRC leo, Jumatano Julai 31,2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa shirika hilo, Jamila Mbarouk imeeleza kuwa taarifa za awali zinaonesha kuwa hitilafu za aina hiyo husababishwa na wanyama (Ngedere) au ndege (Bundi) wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system).
Amesema hitilafu hiyo imesababisha umeme kukatika katika kituo cha kupoozea umeme namba 7 (Godegode) ambayo kitaalamu hujulikana kama (Intanteneous Overcurrent Protection Trip) majira ya saa 04:20 usiku.