MANYARA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Mhe. Jenista Mhagama amewapongeza SUMA JKT kwa hatua nzuri waliyofikia katika ujenzi wa nyumba za makazi kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko ya mawe na matope mwezi Desemba, mwaka jana.
Muonekano wa baadhi ya nyumba zilizojengwa na Serikali kwa wananchi waliokumbwa na maafa ya maporomoko ya matope na mawe Hanang' zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Waziri ametoa kauli hiyo Julai 3,2024 wakati alipotembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa katika eneo la Waret katika Kijijiji cha Gidagamowd Kata ya Mogitu iliyopo Wilaya ya Hanang’.
Muonekano wa baadhi ya Nyumba zilizojengwa na Serikali kwa wananchi waliokumbwa na maafa ya Maporomoko ya Matope na Mawe Hanang zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Ujenzi wa nyumba hizi ni kielelezo cha dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya uzalendo kwa Taifa lake, utu na mapenzi kwa wananchi katika kuwatumikia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za wanachi waliokumbwa na maafa ya Maporomoko ya Matope na mMawe Hanang’ Disemba mwaka Jana.
“Nimefurahi mmerithisha ujuzi wa ujenzi kwa sababu nyumba hizi zimejengwa kwa ubora wa hali ya juu na kuzingatia kanuni za kiuhandisi wakati wa ujenzi,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, ameelekeza kwa uongozi wa Mkoa wa Manyara kuhakikisha miundo mbinu ya Elimu, Soko na Afya inakamilika kwa muda unaotakiwa kama ilivyofanywa katika urejeshaji wa hali kwa kuhakikisha huduma za maji, nishati ya umeme inapatikana sambamba na ufunguaji wa barabara.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi akitoa taarifa ya Maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Nyumba za wananchi waliokumbwa na mafuriko ya Mawe na Matope Hanang’ Disemba mwaka jana.
Waziri Mhagama amesema, “Makazi yanapendeza na baada ya muda Mji huu utakuwa Mkubwa sana na utakuwa Mji wa kihistoria ni vyema tukaendelea kutuna mazingira ili kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi.”
Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mhe. Halimish Issa Hazali akitoa taarifa ya wilaya kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Jensita Mhagama wakati wa ziara yake katika wilaya ya Hanang’.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Mhe. Halimish Issa Hazali amesema Waziri Mhagama ametembelea Nyumba za SUMA JKT nyumba 73 na 1 UWT na ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi na pia ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba 35 zinazosimamiwa shirika la Msalaba Mwekundu.
Nimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya na anaendelea kuifanya kwa wananchi wa Hanang.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama(kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mhe. Halimish Issa Hazali wakipata taarifa kutoka Kaimu Kamanda wa Ujenzi wa Nyumba Luteni Kanali Ashiraf Hassan juu ya maendeleo ya ujenzi nyumba za wanachi waliokumbwa na maafa ya Maporomoko ya matope na mawe Hanang Disemba mwaka jana.
Awali Kaimu Kamanda wa Ujenzi wa Nyumba Luteni Kanali Ashiraf Hassan amesema wamefarijika kwa ziara ya Waziri Mhagama na wamejipanga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na wananchi katika soko jipya lilotengenezwa na Serikali kwa ajili wafanyabiashara wa Hanang’ waliokumbwa na mafuriko ya Matope na Mawe Disemba Mwaka jana.
“Hatuwezi kumuangusha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika adhima yake ya kuhakikisha anawapatia wananchi wa Hanang waliokumbwa na Mafuriko ya Matope na Mawe nyumba bora,” amesema Kaimu Kamanda wa Ujenzi Luteni kanali Hassan.