NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchukua mikopo katika taasisi au watu ambao wamesajiliwa na Serikali huku wakiwa na leseni ya kutoa mikopo ili kuepuka madhila ambayo wanaweza kukumbana nayo.
Wito huo unakuja ikiwa ni rejeo la taarifa iliyotolewa Januari 3,2024 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba ambayo ilifafanua kuwa;
"Benki Kuu ya Tanzania inapenda kukumbusha umma kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, ni kosa kwa taasisi,kampuni au mtu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni.
"Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania haitasita kuwachukulia hatua za kisheria, taasisi, kampuni au watu binafsi wanaofanya biashara ya kukopesha bila ya kuwa na leseni.
"Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 16(2)(a) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018, hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukaji wa Sheria ni pamoja na faini isiyopungua shilingi milioni 20 au kifungo cha muda usiopungua miaka miwili au vyote viwili kwa pamoja.
"Benki Kuu inawakumbusha wakopaji wote kuhakikisha wanasoma mikataba ya mikopo inayotolewa na wakopeshaji, kuelewa na kukubaliana na vigezo na masharti ikiwa ni pamoja na riba na gharama nyingine za mikopo hiyo.
"Tunasisitiza kuwa mkopeshaji anatakiwa kutoa nakala ya mkataba wa mkopo kwa mkopaji, kadhalika mkopaji ana haki ya kudai na kupewa mkataba wa mkopo kila anapochukua mkopo.
"Tunapenda kuusisitizia umma kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye hana leseni kutoka Benki Kuu.
"Aidha,orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zinatolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwenye tovuti yetu ambayo ni www.bot.go.tz," ilibainisha sehemu ya taarifa hiyo ya Gavana Tutuba.
Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:
Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha
Idara ya Usimamizi wa Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha Benki Kuu ya Tanzania
2 Mtaa wa Mirambo, S.L.P 2939 Dar es Salaam
Simu Na. +255-22-223-5585;
Barua Pepe: info@bot.go.tzor botcommunications@bot.go.tz