NA VICKY KIMARO
TUME ya Madini ipo kwenye mchakato wa kuboresha vifungashio vya madini katika masoko ya madini nchi nzima ikiwa ni mkakati wa kuendelea kudhibiti utoroshaji wa madini.
Hayo yamesemwa na Aloyce Bwana ambaye ni Mteknolojia Maabara katika Maonesho ya 48 Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba).

Amesema, mkakati wa Tume kuanzia mwaka huu wa fedha 2024/2025 ni kuhakikisha vifungashio katika masoko yote ya madini vinakuwa vya aina moja tofauti na ilivyo sasa vinatofautiana.
Amesema, kuwa na aina moja ya vifungashio itapunguza utoroshaji wa madini unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu na kuinyima Serikali mapato.


Amesema mpaka sasa Tume ya Madini ina masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 102 nchini ambayo yameongeza mchango wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye mapato kutoka asilimia tano hadi asilimia 40 Mwaka 2022/2023.
Amesisitiza kuwa masoko ya madini yamepunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya utoroshaji wa madini pamoja na kuleta ushindani kwa wafanyabiashara wa madini kupitia masoko na vituo vya ununuzi wa madini.