Wahabeshi 28 wakamatwa Arusha

ARUSHA-Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha usiku wa kuamkia Julai 5,2024 imefanikiwa kukamata raia 28 wa Ethiopia maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kisongo uliopo nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Ni baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema na kushirikiana na vyombo vingine vya usalama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhamiaj, baada ya kuwakamata raia hao kupitia maelezo yao walidai walikuwa wamepakiwa kwenye lori la mizigo ambalo lilipata ajali, baada ya kugongana na gari lingine ndipo wakashuka na kujificha porini maeneo hayo.

Aidha,baada ya kupekuliwa baadhi ya raia hao walikutwa na majeraha kwenye miili yao hasa maeneo ya kichwani yaliyosababishwa na ajali hiyo.

Raia hao waliingia nchini kutokea nchini Kenya kwa lengo la kwenda Afrika ya Kusini kupitia Tanzania, wote waliokamatwa waliingia nchini kinyume cha sheria kwa kuwa hawakuwa na pasipoti za Taifa lao.

"Idara ya Uhamiaji inaendelea kutafuta gari lililotumika kusafirisha raia hao pamoja na wasafirishaji. Tunapenda kutoa wito kwa wananchi kutokujihusisha kwa namna yoyote ile na usafirishaji haramu ya binadamu na pindi watapobaini kwamba wapo raia wa kigeni wanaosafirishwa kimagendo watoe taarifa kwenye vyombo vya doria.

"Ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na pia tunaomba wanachi kutoa ushirikiano kwa Idara ya Uhamiaji na vyombo vingine vya usalama ili kukomesha vitendo vya uhamiaji haramu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news