Wakurugenzi wa Halmashauri jengeni vituo vya bodaboda-Waziri Mchengerwa

NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanajenga vituo vya bodaboda vya kupaki pikipiki vyenye uwezo wa kuzuia jua na kuwakinga na mvua wanaposubiri wateja.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam, wakati akizindua sare maalum (uniform) na mfumo wa kidijitali (kanzidata) wa madereva Bodaboda na bajaji wa jiji la Dar es Salaam.

“Ninaelekeza vituo hivi vijengwe mara moja ili kuwasaidia bodaboda kupata eneo salama la kupaki wakati wakisubiria wateja,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amewahimiza Wakuu wa Mikoa nchini nchi nzima kusimamia uandaaji wa mfumo wa kidijitali (kanzidata) wa kuwatambua madereva Bodaboda na bajaji kama ilivyofanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuwalinda na kuwathamini maafisa usafirishaji hao maarufu kama madereva bodaboda na bajaji, kama ambavyo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza.

Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuweka utaratibu utakaowawezesha maafisa usafirishaji hao kunufaika na mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri ambao unawalenga wanawake, vijana na wenye ulemavu.“Wakurugenzi wa halmashauri wekeni utaratibu mahususi utakaowawezesha maafisa usafirishaji kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri zenu kwa kundi la wanawake, vijana na wenye ulemavu,” Mhe. Mchengerwa amehimiza.

Waziri Mchengerwa ameelekeza mchakato wa kutoa mikopo ya asilimia 10 uanze mara moja ndani ya mwezi huu wa Julai, 2024 ili walengwa wanufaike na mikopo hiyo kama ilivyokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news