NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuacha mara moja kamata kamata ya boda boda isiyo na tija.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo akiwa Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam wakati akizindua sare maalum (uniform) na mfumo wa kidijitali (kanzidata) wa madereva Bodaboda na Bajaji wa jiji la Dar es Salaam.
“Kuanzia sasa sitaki kusikia kamata kamata ya hovyo, inayotokana na wakati fulani kuwepo na sintofahamu baina yenu na maafisa wa Serikali,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa kila mtanzania katika ujenzi wa taifa, wakiwemo madereva boda boda, madereva bajaji, mama lishe na wengineo hivyo haiko tayari kuona yeyote akisumbuliwa au kunyanyasika.
“Mchango wenu ni mkubwa sana hivyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi inawathamini sana ninyi maafisa usafirishaji wa bodaboda na bajaji, na ndio maana ninataka kuona ushirikiano mzuri unakuwepo baina yenu na serikali,” Mhe. Mchengerwa amehimiza.
Ameongeza kuwa, maafisa usafirishaji na maafisa wa serikali wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano katika mikoa na wilaya ili kwa pamoja washiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuwa na utaratibu wa kukutana na vikundi vya boda boda mara kwa kwa mara kwa lengo la kutatua kero na changamoto zinazowakabili, ambazo ndio chanzo cha kufarakana na kuibua migogoro.Mhe. Mchengerwa ameainisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hapendezwi na migogoro inayoibuka baina ya maafisa usafirishaji wa boda boda na Maafisa wa serikali, kwani migogoro hiyo inakwamisha ukusanyaji wa mapato ambayo yanachangia maboresho ya utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta za afya, elimu, kilimo na miundombinu.