NA DIRAMAKINI
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita uliofanyika Mei, 2024 ambapo jumla ya watahiniwa 111,056 wa shule na kujitegemea sawa na asilimia 99.43 ya watahiniwa wenye matokeo ya mtihani huo wamefaulu.
Matokeo hayo yametangazwa leo Julai 13,2024 na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt.Said Mohamed akiwa katika ofisi za baraza hilo jijini Zanzibar.
"Katika mkutano wake wa 160 uliofanyika leo tarehe 13 Julai,2024 katika ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania zilizopo hapa Zanzibar.
"Baraza limeidhinisha kutangazwa rasmi kwa Matokeo ya Kitaifa ya Kidato cha Sita na Ualimu iliyofanyika mwezi Mei,mwaka huu.
"Kuhusu usajili jumla ya watahiniwa 113,536 walisajiliwa wakiwemo wanawake 50,614 sawa na asilimia 45 na wanaume 62,922 sawa na asilimia 55. Kati ya waliosajiliwa watahiniwa wa shule walikuwa 104,454 na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 9,082."
Katibu Mtendaji huyo amesema,wanawake waliofaulu ni 49,837 sawa na asilimia 99.61 wakati wanaume waliofaulu ni 61,219 sawa na asilimia 99.28.
Kwa, mwaka 2023 watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 104,549 sawa na asilimia 99.23, hivyo ufaulu wa jumla mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 0.20 ikilinganishwa na mwaka 2023.
“Watahiniwa wa shule waliofaulu ni 103,252 sawa na asilimia 99.92 ya watahiniwa wenye matokeo, wanawake waliofaulu ni 46,615 sawa na asilimia 99.93 na wanaume ni 56,637 sawa na asilimia 99.91."
Amesema,watahiniwa walioshindwa mtihani ni 84 sawa na asilimia 0.08. “Idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 7,804 sawa na asilimia 93.34, mwaka 2023 watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 8,539 sawa na asilimia 92.30 walifaulu mtihani huo, hivyo ufaulu wa watahiniwa wa kujitegemea umeongezeka kwa asilimia 1.04 ikilinganishwa na mwaka 2023."
Wakati huo huo,Dkt.Mohamed amesema,baraza hilo limefuta matokeo yote ya watahiniwa 22 ikiwa ni 17 wa shule na watano wa kujitegemea ambao walibainika kufanya udanganyifu.
“Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (2) (i) na (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani Mwaka 2016.”