Watoto waende shule, asisitiza Makamu wa Rais

NA JAMES MWANAMYOTO

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kusoma kwa bidii ili taifa lipate viongozi bora wa baadae.
Wito huo ameutoa wilayani Uvinza wakati akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Kigoma.
“Ndugu zangu hili ninalisema kutoka moyoni, hawa watoto hakikisheni wanakwenda shule na mfuatilie kama wanaenda kusoma na si kucheza, na msipowafuatilia hatutopata viongozi bora wa baadae watakaoendana na teknolojia ya kidijitali,” Mhe. Dkt. Mpango amesisitiza.

Dkt. Mpango amesema, hatuwezi kupata madaktari bingwa na wataalam wa kada nyingine kama watoto hawajasoma vizuri na kupata elimu itakayowawezesha kuwa wabobevu katika fani mbalimbali.
“Tunataka madaktari, walimu, wahandisi na viongozi wa ngazi zote ambao watakuwa wemesoma vizuri, hivyo wasimamieni watoto wasome kwa bidii kwani tusipowekeza kwenye elimu tutaendelea kusuasua,” Mhe. Dkt. Mpango amehimiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Mhe. Zainab Katimba amewataka wazazi nchini kumuunga mkono Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha watoto wanakwenda shule na wanapata elimu bora itakayokuwa na manufaa na tija kwa taifa.
“Wazazi jukumu letu kubwa ni kuhakikisha watoto wanakwenda shule, kwani Serikali ya Awamu ya Sita imetumia fedha nyingi kujenga miundombinu bora ya shule za awali, msingi na sekondari ili watoto wa kitanzania wapate elimu bora,” Mhe. Katimba amesisitiza.
Mhe. Katimba ameanisha kuwa, katika mkoa wa Kigoma pekee Serikali imeleta bilioni 82 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu ampazo zimetumika kujenga miundombinu bora na rafiki inayowawezesha watoto kusoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Waende shule kupoteza Muda kisha wanarudi nyumbani na division zero na four mbovu mbovu mbovu
    Hakuna kiongozi hata mmoja anaongelea matokeo mabaya wala ukosefu wa ajira kwa watoto wasio connection hata kama watakomaa kusoma wataishi kuwa bodaboda na degree zao za UDOM
    Maana UDOM inamwaga waendesha bodaboda wenye degree
    Bora UDOM waanzishe degree ya bodaboda kabisa

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news