RUVUMA-Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wamemshukuru na kumpongeza Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha madaraja kila baada ya miaka minne kwa waajiriwa wapya na kwa kila baada ya miaka mitatu kwa walioko kazini.
Wameyasema hayo wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi na kupitia Grupu la Watumishi wa Umma la Wilaya ya Nyasa, baada ya kuona mabadiliko makubwa tangu Mheshimiwa Rais Dkt.Samia aingie madarakani.
Jumla ya watumishi wa umma 823 wamepanda madaraja kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wilayani Nyasa.
Watumishi hao wamefafanua kuwa, kila muda wa kupanda madaraja ukifika wanapanda bila kuuliza wala kufuatilia, hivyo wanampongeza Mhe. Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuboresha maisha ya wafanyakazi yanayopelekea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuongeza kujituma zaidi.
Mwalimu Denis Ndomba wa Shule ya Msingi Matarawe, iliyopo Kata ya Tingi wilayani hapa amesema, "Hakika Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa inastahili pongezi, na watumishi wa Halmashauri ya Nyasa tunamuunga mkono kwa asilimia 100 Mheshimiwa Rais Samia."
Afisa Mtendaji wa Kata ya Linga, Juma Ndimbo amesema, anampongeza Rais Dkt.Samia kwa kusimamia stahiki za wafanyakazi, kwa kupanda madaraja kwa wakati .
”Kwa kweli inapendeza bila kufuatilia unakuta tayari umepanda daraja, kwa kweli Serikali inafanya kazi nziri ya kuwajali watumishi wake tunahakikisha tunatatua kero za wananchi na kutoa huduma bora kama tunavyopata sisi.”
Pia wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa,Bw. Khalid Khalif na Divisheni ya Utawala na Raslimali watu kwa kuhakikisha kuwa, kila anayestahili kupanda cheo anapanda kwa wakati na kutekeleza kwa wakati maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunaona wakati wa zoezi la kupandisha madaraja Mkurugenzi na timu yake wanafanya kazi usiku na mchana ili kutoa huduma bora kwa wafanyakazi wake tunampongeza sana.”
Watumishi wamemuahidi Mheshimiwa Rais kuwa watatekeleza majukumu yao ipasavyo na kuongeza bari ya kuchapa kazi na kumuung mkono kwa kutangaza mazuri.