ZANZIBAR-Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amesema uzalishaji wa sukari kwa Tanzania Bara umeongezeka kwa kiasi kikubwa zaidi ya miaka iliyopita na ili kukidhi mahitaji yaliyopo kupitia kampuni za sukari inatarajiwa kuzalishwa tani 706,000 ifikapo mwaka 2025/26.
Akizungumza leo Julai 10, 2024 kwenye Mkutano wa wazalishaji wa sukari wa nchi Wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) SADC uliofanyika Zanzibar, Dk. Jafo amesema mkakati uliopo ni viwanda viendelee kufanya vizuri kwenye uzalishaji sukari ili kukidhi mahitaji ambapo kwa mwaka 2023/24, mahitaji ya sukari Tanzania yalikuwa takriban tani 807,000.
Amesema,kati ya hizo tani 552,000 ni kwa ajili ya matumizi ya ndani na tani 255,000 zilizobaki zimetengwa kwa matumizi ya viwandani.
“Tanzania Bara uzalishaji wa sukari umeongezeka kwa kiasi kikubwa zaidi ya miaka iliyopita ambapo uzalishaji wa sukari kwa mwaka 2023/24 ulikuwa takriban tani 470,000. Ili kukidhi mahitaji ya sukari, Serikali ya Tanzania kupitia kampuni zake zinazozalisha sukari iliamua kuongeza uzalishaji wa sukari kwa asilimia 53.5, na tunatarajia kuzalisha tani 706,000 ifikapo mwaka 2025/26,”amesema.
Amesema mafanikio hayo ni ya kujivunia kama taifa ni kuwa na mkakati sukari ya kutosha katika siku za usoni, kwa matumizi ya hapa nchini na ziada kwa usafirishaji.
“Nchini Tanzania, sekta ya sukari ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na fursa ya ajira kwa wafanyakazi wa viwandani na wakulima.
Sekta ya sukari ni sekta muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi na maisha ya watu wetu,”alisema.
Amepongeza jukumu kubwa lililofanywa na kampuni sita zinazozalisha sukari, ambazo ni Tanganyika Planting Company Limited, Kilombero Sugar Company Limited,Kagera Sugar Limited, Mtibwa Sugar Estates Limited, Mkulazi Holding Company Limited na Bakhresa Sugar Limited.
Aidha,amesema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iliridhia mpango mkakati wa SADC wa sekta za viwanda ambao utekelezaji wake umeanza Mwaka 2015 hadi 2063.
Naye, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaabani alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa sekta ya sukari katika maendeleo ya viwanda na maendeleo ya uchumi wa nchi.
Alisema, jukwaa hilo limewakutanisha wadau wa sekta ya sukari kwa kubadilishana mawazo na uzoefu kwa lengo ni kuchangia katika maendeleo endevu ya sekta ya sukari katika jumuiya ya SADC.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Prof. Kenneth Bengesi, alisema kongamano hilo muhimu kwani wataweza kubadilishana uzoefu wazalishaji hao katika tathnia ya sukari ili kuelekea ushindani wa sukari Afrika.Alisema ni muhimu kuwa na sera na sheria zilizobadilika mara kwa mara kufanya hivyo kutasaidia kuleta mvuto katika sekta hizo kwa kuhakikisha wanatoa fursa nzuri ili vijana vipate ajira kupitia biashara hiyo.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni "Kuendeleza sekta ya sukari yenye ushindani barani Afrika" (Towards a Competitive Sugar Industry in Africa).