Waziri Jafo apongeza utendaji kazi wa Wakala wa Vipimo (WMA), ataka wengine waige mfano

NA VERONICA SIMBA
WMA

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo, amepongeza Wakala wa Vipimo (WMA) kwa utendaji kazi mahiri na wenye weledi na kutoa wito kwa Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara hiyo kuiga mfano wake.

Ametoa pongezi hizo mapema leo, Julai 17, 2024 jijini Dodoma alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Wakala huo, lililopo eneo la Medeli.
Mheshimiwa Jafo amekiri kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na utendaji kazi wa WMA kupitia ziara zake alizofanya kukagua kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Wakala huo, ambapo awali (Julai 11, 2024) alitembelea Kituo cha Uhakiki wa Vipimo kilichopo Misugusugu Mkoa wa Pwani na kujionea utendaji kazi wake.

“Kwa ujumla nimeridhishwa sana na utendaji wa Wakala huu na niwatake wengine waige mfano huu mzuri. Wito wangu, waendelee kufanya kazi kwa lengo la kuhakikisha Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inapata mafanikio makubwa katika maeneo yote,” amesema.

Ameongeza kusema kuwa, pongezi zake kwa Wataalamu wa Wakala wa Vipimo pia ni kutokana na kuonesha mfano mwema sana kwa kutumia mapato ya ndani, kujenga jengo hilo, hali inayothibitisha kuwa Taasisi hiyo ni miongoni mwa zile zinazofanya vizuri.

Akieleza zaidi, Waziri Jafo amesema lengo la ziara yake kukagua jengo hilo ilikuwa kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha iliyowekezwa katika ujenzi huo pamoja na kasi ya utekelezaji wake ambapo kwa ujumla amesema ameridhishwa kwa kiasi kikubwa.

Akifafanua, amesema kuwa, kwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi, ambayo ni asilimia 81.5 anaamini jengo hilo linaweza kukamilika hata kabla ya muda uliopangwa ambao ni Januari 2025.Hata hivyo, pamoja na kumpongeza Mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo, Kampuni ya M/S Mohamed Builders chini ya Mshauri Elekezi, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), amewataka kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kwa wakati na viwango stahiki kama inavyotarajiwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Jafo amewasisitiza watendaji wa WMA kuzingatia maelekezo aliyoyatoa kwao katika ziara yake ya awali, kuhusu kukagua maeneo yote yanayohusu ukaguzi hususani mita za umeme na maji kabla hazijafungwa kwa wateja ili kulinda haki za walaji ambao ni wananchi.

“Naelekeza mita zote za umeme na maji lazima zifikishwe Wakala wa Vipimo ili kuzipima kuangalia uthibiti wake kwa lengo la kuwapunguzia gharama wananchi. Isije mtu akafungiwa mita ambayo haina ubora, mwisho wa siku akalipa bili isiyo stahiki,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Joseph Maliti ametoa ahadi kwa Waziri kuwa Wakala utahakikisha maelekezo yake yote yanatekelezwa.

Naye Mwakilishi wa Mkandarasi, Mhandisi Justin Kyando amesema wana uhakika watakamilisha ujenzi kwa wakati kwani wako katika hatua za ukamilishaji.

Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo jijini Dodoma ulianza Julai 2, 2022 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025 ambapo gharama yake ni shilingi bilioni 6.17.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news