Waziri Makamba aongoza ujumbe wa Tanzania mkutano wa 26 wa MCO-SADC

LUSAKA-Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO) wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai, 2024 ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Yusuph Makamba ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano huo.Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika kuanzia tarehe 08 hadi 09 Julai 2024 ambapo kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliwakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Amani Mashaka kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 25 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC, Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda, na Uimarishaji wa Demokrasia katika Kanda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha nchini Zambia wajumbe wa mkutano huo ambao agenda yake kuu ni kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa SADC na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana kwenye maeneo yenye changamoto.

Aidha, akizungumzia hali ya amani na usalama kwenye maeneo yenye changamoto hususan eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho na eneo la Kaskazini mwa Msumbiji, Dkt. Haimbe amesema hali sasa inatia moyo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha amani, usalama na utulivu wa kudumu vinapatikana kwenye maeneo hayo ili kuwa na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika kanda.

Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Mpedi Magosi amesema kuwa, Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi ili hatimaye kuwa na Kanda tulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi, Mhe. Daniel Sillo (Mb), Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Amani Mashaka kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi Sudi Mwakibasi na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamehudhuria Mkutano huo.

Ikumbukwe kuwa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua Uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news