Waziri Mavunde aagiza leseni 45 za utafiti mkoani Rukwa zirejeshwe serikalini

RUKWA-Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Serikali imefuta na kuzirejesha Leseni za Utafiti wa Madini 45 kati ya 102 zilizopo mkoani Rukwa kwa kushindwa kufanyiwa kazi na kukidhi masharti yaliyowekwa.Waziri Mavunde aliyasema hayo Julai 16, 2024 wilayani Sumbawanga, wakati akijibu hoja za Uongozi wa Wachimbaji mkoani Rukwa kuhusu ombi la kupatiwa maeneo ya uchimbaji katika kikao kilichofanyika baina ya Waziri wa Madini na wadau wa Sekta ya Madini mkoani humo.“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo bayana ya kuhakikisha Leseni zinatolewa zinafanya kazi na watu wasihodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi ili kuchochea shughuli za uchimbaji na ukuaji wa sekta ya madini.

"Hapa Mkoani Rukwa tumerejesha Leseni 45 Serikalini ili kutoa fursa kwa Serikali kuyapanga vyema maeneo hayo kwa kutenga Leseni kwa ajili ya wachimbaji wadogo na wawekezaji wakubwa walio tayari kuwekeza kwenye sekta ya madini,” alisema Mhe. Mavunde.
Aliongeza kuwa, Leseni hizo 45 zilikuwa zimeshikilia eneo kubwa la ekari 812,383 ambalo ni kubwa kuliko eneo lote la Wilaya nzima ya Sumbawanga ambayo ina eneo la ukubwa wa ekari 667,641.

Vilevile, Waziri Mavunde alisema kuwa shughuli za uchimbaji mkoani Rukwa bado zipo chini, na kwamba ni jukumu la Ofisi ya Afisa Madini Mkoa kuhakikisha inachochea shughuli za uchimbaji mkoani humo.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Joseph Kumburu alimuhakikishia Waziri Mavunde kuwa atasimamia utekelezaji wa maagizo hayo hasa la kuchochea shughuli za uchimbaji wa madini kwa kuwa Rukwa imejaaliwa madini mengi ya aina tofauti tofauti na kwamba una fursa kubwa ya kufanya vizuri zaidi.
Awali, akiwasilisha taarifa ya Wachimbaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Mkoani Rukwa (RUREMA),Masie Mwambegele aliiomba Serikali kuwapatia maeneo Wachimbaji Wadogo katika maeneo ambayo hayafanyiwi kazi na kuomba Serikali kuongeza nguvu kwenye eneo la utafiti ili wachimbaji wasichimbe kwa kubahatisha kama ilivyo sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news