DODOMA-Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ametoa zuio kwa raia wote wa kigeni kuingia kwenye leseni za uchimbaji mdogo (PML)bila kufuata taratibu zilizoelezwa kwenye Kifungu cha 8 cha Sheria ya Madini Sura ya 123.

"Dhamira ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona nchi inaongeza uwekezaji lakini unaofuata taratibu na pia kwa upande wa pili kuona wachimbaji wadogo wananufaika na rasilimali madini kupitia shughuli za uchimbaji,"amesema Waziri Mavunde.
Ameongeza kwamba,leseni za uchimbaji mdogo ni kwa ajili ya Watanzania, hivyo hatarajii kuona raia wa Kigeni anaingia kwenye leseni hizo pasipo makubaliano maalum ya msaada wa kiufundi ambayo yamesajiliwa na Tume ya Madini.
Kutokana na migogoro mingi inayojitokeza baina ya mwenye leseni na wachimbaji wadogo wenye maduara, zimeandaliwa Kanuni ambazo zimeweka masharti kwa mmiliki wa leseni kuzuia wachimbaji wadogo kuchimba ndani ya Leseni yake au ikiwa ametoa ridhaa basi ni sharti ni kuingia mkataba na wote wanaochimba katika leseni yake ili kulinda maslahi yao na kuwaelekeza maafisa madini nchi nzima kufanya operesheni ya ukaguzi wa mikataba ya msaada wa kiufundi.
"Pia, naagiza Afisa Madini wote nchini kuhakikisha wamiliki wote wa leseni za kubwa za Biashara ya madini (Dealer Licence) hawaendi moja kwa moja kwa kwenye maeneo ya uchimbaji na badala yake waende kwenye masoko ya madini kama masharti ya leseni yao," amesema Waziri Mavunde.

