Waziri Mavunde awataka watumishi wa wizara kufanya mazoezi

DODOMA-Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (MB) ameelekeza watumishi wa Wizara na Taasisi zote zilizopo chini ya Wizara yake ikiwemo Tume ya Madini kuhakikisha wanafanya mazoezi ili kupambana na magonjya yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari, moyo na shinikizo la damu.
Pia, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kuandaa Bonanza maalum litakalokutanisha watumishi wote wa Wizara ya Madini na Taasisi zake ikiwemo Tume ya Madini pamoja na Wadau wa Madini.Picha zaidi tazama hapa》》》

Mhe. Mavunde ametoa maelekezo hayo Julai 6, 2024 katika Bonanza Maalum lililoandaliwa na Tume ya Madini, lililofanyika kwenye viwanja vya Kilimani jijini Dodoma.

Amesema, bonanza hilo maalum ambalo linafanyika kila mwaka lina lengo la kuwaleta pamoja kama wafanyakazi chini ya tume.

“Inawezekana wengine mnakutana kwenye Makorido na kazi zenu sio za kuwafanya mkakutana kila siku, lakini michezo inawaleta pamoja,”amesema Mhe. Mavunde na kuongeza,

“Lakini pia kama mnavyofahamu hivi sasa kuna changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza kama Kisukari, Presha na mangonjwa mengine, tumepata maelekezo ya wataalam wetu kufanya mazoezi ili kuondokana na changamoto hii, nawapongeza Tume, imekuwa ikifanya Bonanza hili kwa miaka minne sasa na aliyekuwa analiasisi ni ndugu yangu Katibu Mkuu, Mhandisi Yahya Samamba, ninaamini umekwenda Wizarani usilifanye la Tume peke yake, nategemea siku moja nione Bonanza kubwa litakalokutanisha taasisi zetu zote GST, Stamico, TEITI lakini pia mlete na wadau, wachimbaji wadogo na wakubwa wote tuwepo hapa" amesisitiza Mhe. Mavunde.

“Tukae hapa siku moja tufanye Bonanza hili na wote tufurahi, naamini lipo ndani ya uwezo wako, utalifanya na utalisimamia kikamilifu,”amesema Mhe. Mavunde.

Aidha, amewapongeza watumishi wote wa Tume ya Madini walioshiriki Bonanza hilo ambalo lilipambwa na michezo mbalimbali ikiwemo kufukuza kuku, kuvuta kamba na mpira wa miguu ambapo washindi wamepata medali na tuzo.

“Washindi wote ambao wamefanya vizuri nawapongeza naamini hii ni chachu kwa watumishi wengine kufanya vizuri kwenye mashindano yanayokuja,” amesema Mhe. Waziri Mavunde.

Awali, akizungumza Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesema mazoezi ni muhimu kwa kuwa yanaimarisha afya ya akili na umoja kwenye sehemu za kazi na kuwataka Watumishi waendelee kuwa wabunifu kwenye kazi zao ili kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Amesema, ni muhimu kwa Watumishi wa Tume ya Madini kuimarisha Bonanza kwa kupanda Mlima Kilimanjaro.

“Kuna msemo unasema michezo ni umoja, michezo ni ajira, michezo inaleta watu pamoja, inaondoa tofauti, michezo inajenga ushirikiano na ‘teamwork spirit’ katika taasisi yetu, michezo ni afya ni burudani, amesema Mhe. Naibu Waziri na kuongeza,

“Michezo sio lazima uwanjani panueni wigon kwa kupanda mlima Kilimanjaro tukahamasishe ajenda yetu ya vision 2030 tukishirikisha watanzania na wadau wote wa madini na kuhitimisha kwa kusema kuwa,

“Lengo ni kila mtu ashiriki atakaetembea kilomita tano, kumi atakaefika kileleni mradi ni kujenga hamasa kubwa, kuhamasisha taifa kupitia sekta yetu ya madini watanzania wazijue fursa zilizopo na washiriki kuzichangamkia au tukahamasisha kupinga utoroshwaji wa madini nchini,"amesema Mhe. Dkt.Kiruswa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news