Waziri Mhagama atoa kongole kwa DCEA

ARUSHA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu,Mhe.Jenista Mhagama ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa kazi nzuri inayofanyika katika kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Ameeleza kuwa, waka 2023 mamlaka ilipata mafanikio makubwa kwa kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho ni mara tatu ya kiasi kilichowahi kukamatwa hapa nchini kwa zaidi ya miaka 11.
Mheshimiwa Mhagama ametoa pongezi hizo leo Julai 31,2024 jijini Arusha wakati akifungua kikao cha mazingativu kinachojumuisha watumishi kutoka taasisi zote zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa, kazi hiyo kubwa ya kuokoa jamii hususani vijana kundi ambalo linaathiriwa zaidi na dawa za kulevya, imetokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali, uzalendo na juhudi kubwa za viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

"Niwapongeze sana, lakini pia tunatakiwa kuendelea kusimamia kwa karibu vita dhidi ya biashara haramu ya matumizi dhidi ya dawa za kulevya.
"Na hapa pia naomba nitoe kongole kwa mamlaka kwa kazi kubwa ambayo imefanyika na sisi sote ni mashahidi."

Amesema, mamlaka hiyo imeonesha ufanisi mkubwa katika udhibiti na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya nchini.

"Ukamataji uliofanywa kwa mwaka 2023 ni zaidi ya mara tatu na zaidi ya ukamataji uliofanywa kwa kipindi takribani miaka 11 iliyopita.

"Na hii si kwa sababu, labda kumekuwa na ongezeko kubwa, hapana ni kwa sababu kwanza Serikali imeamua kuwekeza kwenye mamlaka.

"Lakini, kikubwa ni uzalendo wa mamlaka yetu katika kufanya kazi hii muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu.
"Lakini, kwa hili ninawapongeza sana. Serikali imewekeza rasilimali watu, imewekeza vitendea kazi na wao wameweza kutendea haki majukumu yao.

"Hivyo, tuna kila sababu ya kuwaomba mamlaka waendelee kusonga mbele katika kuhakikisha biashara haramu ya dawa za kulevya inakomeshwa hapa nchini."

Amesema, nguvu kazi kubwa iliyopo hapa nchini ni vijana. "Lakini, tafiti zinasema kijana mmoja akila kete moja ya Cocaine ama Heroine ama bangi inachukua saa sita kuwa katika hali ya kupoteza fahamu,

"Uwezo wa kufikiri, uwezo wa kufanya kazi, uwezo wa kujitambua na uwezo wa kuchangia jambo lolote ambalo linakuwa na tija kwa ustawi wa Taifa sasa tupate picha kama biashara hii hatutapigana nayo kwa nguvu zote, vijana wengi wakajiingiza katika matumizi hayo.

"Kwa hiyo, tutakuwa na kundi la vijana kila siku na kwa mujibu wa utafiti kijana mmoja anakuwa na uhitaji wa kete zaidi ya moja, mbili mpaka tatu kwa siku.
"Kwa hiyo atakuwa na saa sita ya kutokuwa na tija na atakapopata unafuu anaongeza saa sita ya pili tena za kutokuwa na tija na akipata nafuu anaongeza saa sita nyingine.

"Kwa maendeleo na ustawi wa Taifa ni hatari, kwa hiyo kongole kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mnatutendea haki, mnaokoa nguvu kazi ya Taifa ambayo inatakiwa ifanye kazi ya kuleta maendeleo endelevu kwenye Taifa letu,"amesisitiza Waziri Mhagama.

Pia,ameagiza sera mpya ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ianze kufanya kazi ili iweze kuleta tija kubwa zaidi katika udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news