Waziri Mhagama awataka wananchi kuwekeza katika elimu

RUVUMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu),Mhe. Jenista Mhagama (Mb) na Mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma amewataka wananchi wa Muhukuru Lilahi kutumia fursa iliyopo kuwapeleka vijana wao kujiunga katika Chuo cha Maendeleo ya jamii kilichopo katika eneo hilo ili kunufaika na maarifa na ujuzi mbalimbali unaotolewa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akiwasha umeme katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Kilichopo Kitongoji cha Aboud Jumbe Muhukuru-Lilahi.

Waziri ametoa kauli hiyo Julai 16,2024 wakati wa hafla ya uwashaji wa umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Kitongoji cha Aboud Jumbe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma ambapo umeme umewashwa katika Chuo hicho cha Maendeleo ya Jamii.
"Umeme utasaidia utoaji wa mafunzo ya ufundi katika chuo hiki kuwa bora na ya kisasa zaidi na matokeo yake ni kuandaa vijana wetu kuweza kujiajiri na kuongeza fursa zao za kuweza kuajiriwa.

“Vijana wana nafasi ya kutoa mchango mkubwa sana katika ujenzi wa taifa unaohitaji ujuzi wa kisasa unaoendana na mafunzo yatakayotolewa katika chuo hiki ndio maana nasema umeme ni elimu,” alifafanua Waziri Mhagama.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akikagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la wavulana katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Kilichopo Kitongoji cha Aboud Jumbe Muhukuru-Lilahi.

Aidha, amewapongeza vijana waliojiunga na Chuo hicho cha Maendeleo ya Jamii kwa kuwa hawajakosea kufanya maamuzi ya kuja kusoma happ kwa sababu wanaelewa umuhimu wa elimu.

“Niendelee kuwahamasisha wananchi wa Muhukuru-Lilahi kuitumia fursa hii vyema, Chuo hiki ni uchumi na chuo hiki ni maendeleo ndio maana kinaitwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii.

"Nimemuachia maelekezo Mkuu wa Chuo atengeneze utaratibu na mkakati maalumu kwa vijana wetu kujiunga na chuo hiki nami nitachangia tupate watoto 10 watakaosoma hapa ili wapate elimu ya ujuzi,"alieleza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Mhe. Menace Komba na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Vijijini na Mhe. Simoni Kapinga wakati wa mkutano wa hadhara Muhukuru-Lilahi.

Awali Diwani wa Kata ya Muhukuru-Lilahi na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Vijijini,Mhe. Simoni Kapinga amesema, chuo hicho kinajihusisha na masuala ya kilimo na mifugo hivyo ameomba Serikali kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kufundishia vya kisasa ili wananchi nao wahamasike kulima kilimo cha kisasa.

“Kupitia wewe Waziri wa Nchi tunaomba utusaidie tupate gari kwa ajili ya chuo hiki kwa kutusaidia kuzungumza na Waziri mwenye dhamana,” alisema Mhe.Kapinga

Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea,Mtela Mwapampamba amewaomba wananchi wa Mhukuru-Lilahi kuacha tabia ya kuuza maeneo kiholela kwa sababu wageni wataongezeka, kutokana na mipango ya ujenzi wa kiwanda cha sukari kinachotarajiwa kujengwa katika kijiji jirani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu),Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa (REA) wakati hafla ya kuwasha umeme katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Muhukuru-Lilahi.

“Maeneo yetu ya uzalishaji tuliyobaki nayo kwa sasa tuendelee kuyatunza kwa sababu yatatufaa sasa na siku za usoni kutokana na mabadiliko makubwa ya miundo mbinu yanayotarajiwa kutokea,"alisema Katibu Tawala Mwampamba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news